Na Silivia Amandius
Bukoba.
Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) imeendesha safari ya majaribio ya pili ya meli mpya ya MV Mwanza, safari iliyoanzia katika Bandari ya Mwanza kuelekea Bandari ya Bukoba kupitia Kemondo, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kuanza safari rasmi za kibiashara.
Safari hiyo ya matazamio imefanyika kwa lengo la kujiridhisha na ubora, uimara na usalama wa meli hiyo kabla ya kuanza kutoa huduma rasmi kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa.
Akizungumza baada ya meli hiyo kutia nanga katika Bandari ya Bukoba, Kaimu Meneja wa Usajili na Ukaguzi kutoka Wakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mhandisi Said Kaheneko, amesema safari ya awali ya majaribio ilibaini baadhi ya changamoto, ikiwemo meli kutoa sauti kubwa.
“Tuliona ni muhimu kufanya jaribio la pili kwa kuijaza meli kwa nusu ya uwezo wake, tukiwa na abiria na mizigo, ili kuhakikisha kila kitu kiko sawa kabla ya kuanza safari rasmi,” alisema Mhandisi Kaheneko.
Kwa mujibu wa taarifa za TASHICO, meli hiyo ilianza safari kutoka Mwanza saa 4 usiku na kufika Kemondo saa 11 alfajiri kabla ya kutia nanga Bukoba majira ya saa 1 asubuhi, ikiwa imebeba abiria 414 na mizigo yenye uzito wa tani 78.6. Meli hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo ya tani 400.
Afisa Uhusiano wa TASHICO, Bw. Abdulrahmani Salim, amesema safari hiyo ya leo ilikuwa ni ya majaribio na siyo ya kibiashara, ikilenga kukagua utendaji wa meli hiyo chini ya mazingira halisi.
“Tunapenda kuwahakikishia wananchi kuwa safari rasmi zitaanza muda si mrefu. Tumeona mwitikio mzuri wa wananchi, na tunakaribisha wote kuchangamkia fursa hii ya usafiri wa kisasa na salama,” alisema Bw. Salim.
Baadhi ya abiria waliopanda meli hiyo wameelezea furaha yao, wakisifu ubora wa meli hiyo na huduma zinazotolewa ndani yake.
“Ni meli kubwa, nzuri na ya kisasa sana. Kwa kweli nimefurahia kusafiri nayo. Meli kama hizi tulikuwa tunaziona tu kwenye nchi nyingine,” alisema Bw. Aniset Saulo, mmoja wa abiria waliokuwa wakielekea Mwanza.
Kwa sasa, TASHICO inaendelea na hatua za mwisho za maandalizi kabla ya kuanza safari za kibiashara za MV Mwanza, meli ambayo inatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri majini katika Ziwa Victoria na kuchochea ukuaji wa biashara kati ya mikoa ya Mwanza, Kagera na maeneo jirani.