*Huduma ya umeme kwenye vitongoji yafikia asilimia 58
*Majiko banifu 200,000 kuuzwa kwa ruzuku ya 80% hadi 85% Tanzania bara
*Mitungi ya gesi 452,455 ya kilo 6 kuuzwa kwa ruzuku ya 50%
*Mifumo 20,000 ya umeme jua kufungwa kwa wakazi maeneo ya visiwani
*Serikali kupitia REA kutoa mikopo ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta
*Watumishi REA waipamba wiki ya huduma kwa wateja
Dodoma
Serikali imeeleza mafanikio makubwa ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji ambapo Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imefanikiwa kufikisha huduma ya umeme kwenye vijiji vyote 12,318 sawa na asilimia 100 na miradi ya umeme kwenye vitongoji inatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2030.
Mafanikio ya miradi ya umeme Vijijini yamebainishwa leo Oktoba 8, 2025 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Umeme Vijijini Mha. Jones Olotu wakati akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa Wiki ya Huduma kwa Wateja jijini Dodoma.
“Tanzania bara tuna jumla ya vitongoji 64,359 ambapo kati ya hivyo vitongoji 37,328 sawa na asilimia 58 vimeshafikiwa na huduma ya umeme na bado miradi ya kusambaza na kufikisha huduma ya umeme inaendelea katika maeneo mbalimbali nchini,” Amesema Mha. Olotu.
Halikadhalika, Mha. Olotu ameongeza kuwa, Wakala wa Nishati Vijijini unatarajia kukamilisha utekelezaji wa kusambaza umeme kwenye maeneo ya vitongoji ifikapo mwaka 2030 ili watanzania wapate huduma ya umeme ili kukuza maendeleo yao binafsi na uchumi wa Taifa.
Katika hatua nyingine, Mha. Olotu amesema Serikali imepata watoa huduma kwa ajili ya kufungwa mifumo ya umeme jua kwa wakazi wa maeneo ya visiwani Tanzania bara ipatayo 20,000.
Katika hatua nyingine, Mha. Olotu amewaasa wananchi kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia REA hususan nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kujikinga na madhara ya kiafya, kimazingira na kiuchumi yanayotokana na matumizi ya nishati isiyo safi na salama.
Vilevile, Serikali kupitia REA inaendelea kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta maeneo ya vijijini ili wananchi waweze kuhifadhi salama bidhaa za mafuta.
Watumishi wa REA wameipamba Wiki ya Huduma kwa Wateja ambayo inafanyika katika ofisi ya Wakala wa Nishati Vijijini makao Makuu jijini Dodoma.