Na Philomena Mbirika, Seville-Hispania
Tarehe 8 Oktoba, 2025
Maonesho ya Tourism Road Show yaliyoanza tarehe 6 Okoba, 2025 nchini Hispania yamemalizika leo tarehe 8 Oktoba, 2025 katika jiji la Seville, yakihitimisha ziara ya siku tatu iliyofanyika katika majiji ya Barcelona, Madrid na Seville kwa kukutana na mawakala wakubwa wa Utalii kwa lengo la kudani vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji.
Maonesho hayo yaliyowakutanisha mawakala wa safari za kitalii takribani 100 kutoka Hispania yametoa fursa kwa Tanzania kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuendelea kushika Soko la utalii barani Ulaya ambapo ni soko la kimkakati.
Mkurugenzi wa chama cha wakala wa usafiri Hispania Bw. Oscar Gabaldòn ambaye pia ni mwakilishi wa Tanganyika expedition nchini hapo, alisema kwamba lengo la kuandaa road show hiyo ni kutokana na mwamko wa watalii nchini hapo kupendelea kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo Tanzania.
“Tanzania ni nchi yenye uzuri wa kipekee ambayo imebarikiwa vivutio vya wanyamapori, utamaduni, fukwe nzuri, Milima ya kuvutia ambavyo nyote hivi vinafanya urahisi kwenye Soko la utalii hapa nchini na ndani ya bara la ulaya kwa ujumla” Alisema Oscar
Kwa upande wa washiriki kutoka Ngorongoro na TANAPA wameleza kuwa kupitia maonesho hayo wamepata fursa ya kuuza vivutio vya Utalii pamoja na fursa za uwekezaji zilizo ndani ya maeneo yanayosimamiwa na taasisi hizo kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii nchini na kuwezesha kufikia lengo la taifa la watalii milioni nane (8) ifikapo mwaka 2030.