Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Moshi, Kilimanjaro – Moto mkubwa ambao chanzo chake bado hakijafahamika umeharibu kabisa vyumba 12 vya makazi na viwili vya biashara katika mtaa wa Dar es Salaam Street, Kata ya Kiusa, ndani ya Manispaa ya Moshi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi, tukio hilo limetokea leo tarehe 11 Oktoba 2025. Hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa, lakini mali zote zilizokuwepo ndani ya nyumba hizo zimeteketea.
“Tulipokea simu ya dharura kuhusu moto uliokuwa ukiwaka katika mtaa wa Dar es Salaam Street. Tulipowasili tulikuta moto tayari umesharipoti katika nyumba 12 za makazi na vyumba viwili vya biashara,” alisema Kamanda Mkomagi.
Aliongeza kuwa katika nyumba hizo hakukuwa na watu wazima wakati tukio linatokea, bali walikuwepo watoto wawili waliogundua moto na kukimbilia kwa jirani kuomba msaada. Ndipo majirani walipotoa taarifa kwa kikosi cha zimamoto.
“Bahati nzuri tulifanikiwa kuuzuia moto huo usisambae kwenye nyumba nyingine zilizokuwa karibu, kwa msaada wa kikosi cha zimamoto kutoka kiwanda cha sukari cha TPC,” aliongeza Kamanda huyo.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Bi Lightness Meada, alieleza namna walivyoshindwa kuuzima moto huo kwa kutumia vifaa vya kawaida hadi kikosi cha zimamoto kilipofika.
“Mtoto alikuja mbio akisema kuna moto nyumbani kwao, tulipokwenda tukaona moto tayari umeshatawala nyumba yote. Tuliwa na juhudi kubwa kuuzima lakini haukudhibitika. Hakuna kilichookolewa,” alisema kwa masikitiko.
Tukio hilo linaendelea kuchunguzwa ili kubaini chanzo halisi cha moto huo ambao umeacha familia kadhaa bila makazi.