
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yupo tayari kuendelea kufanya mambo makubwa kwa watu wenye ulemavu ili kukuza ustawi wa jamii hiyo kwa kuwawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Amesema hayo Oktoba 11, 2025 wakati wa hafla ya kupokea tuzo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia ya ya kutambua mchango wake katika kusimamia ustawi wa jamii ya watu wenye ulemavu nchini, kwenye hafla iliyofanyika kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay Jijini Dar es Salaam. Tuzo imetolewa na taasisi ya Foundation for Disabilities Hope (FDH)
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameahidi kuendelea kuwahudumia watu wenye ulemavu kwa kuwa ana nia ya dhati ya kuona jamii hiyo inakuwa na ustawi utakaowawezesha kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi. “Rais wetu anataka kuona watu wenye ulemavu wanafanya mambo kwa uhuru mkubwa”
“Ndugu washiriki, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mengi sana,nataka niwaambie amenihakikishia kuwa yupo tayari kuendelea kufanya mambo mengi zaidi, niwaombe watanzania wote tuendelee kumuunga mkono”
Amesema kuwa Serikali katika kutekeleza dhamira ya Rais Dkt. Samia ya yakuinua ustawi wa watu wenye ulemavu imeendelea kutekeleza mipango, mikakati na afua mbalimbali ikiwemo kufufua Mfuko wa Taifa kwa Watu wenye Ulemavu ambao tangu ulipoanzishwa mwaka 2010 haukuwahi kufanya kazi.
“Mwaka 2022 serikali ya awamu ya sita imetoa shilingi bilioni 2.1 nahivyo kuwezesha Mfuko huo kutoa ruzuku inayofikia shilingi milioni 408 kwa miaka miwili mfululizo kwa vyama vya watu wenye ulemavu na Shirikisho la SHIVYAWATA”
Ameongeza kuwa Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 8 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa visaidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule za msingi na sekondari. “Vifaa hivyo ni kwa ajili ya Wanafunzi wenye Ulemavu wa kutoona na uoni hafifu, viziwi, Ualbino na wenye ulemavu wa viungo, vifaa vya kufundishia pamoja na vya michezo”
“Serikali kupitia mikopo inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri imetoa shilingi bilioni 16.4 ambayo ni asilimia mbili inayotengwa kwa Watu wenye Ulemavu kwa vikundi na mtu mmoja mmoja mwenye ulemavu. Lengo nikuwawezesha watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi” Alisema Mheshimiwa Majaliwa.
Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete amesema kuwa tuzo hiyo inabeba mrejesho wa shukrani kwa kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Rais. Dkt Samia ameifanya kwa watu wenye Ulemavu katika kipindi cha miaka yake minne ya uongozi.
“Katika kipindi cha uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, tumefanikiwa kufungua milango ya upatikanaji wa ajira kwa watu wenye ulemavu, ambapo zaidi ya Wenye Ulemavu 1213 wameajiriwa katika taasisi mbalimbali za Serikali katika kada za afya, elimu, uhasibu, Lishe na Maendeleo ya Jamii”
Aidha, Mheshimiwa Kikwete amesema kuwa Serikali imetoa ruzuku ya shilingi milioni 61 kwa Kiwanda cha KCMC Moshi Kilimanjaro kuimarisha uzalishaji wa mafuta ya kinga ya saratani ya ngozi kwa watu wenye ualbino kwa gharama nafuu. “Mafuta hayo yamezalishwa na kusambazwa katika vituo vyetu vya afya kupitia Bohari Kuu ya Dawa na yanatolewa bila malipo katika Vituo vya Afya vya Serikali”.
Naye, Mkurugenzi wa Taasisi ya Foundation for Disabilities Hope Michael Selali amesema kuwa watu wenye Ulemavu wameamua kutoa tuzo hiyo kutokana na jitihada za ujumuishi zinazofanywa na Rais Dkt. Samia kwa ajili ya watu wenye Ulemavu ambazo zimewawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi
“Katika jitihada za kuinua Wenye Ulemavu kiuchumi, Serikali imeweza kuanzisha program za ujumuishi kwa watu wenye ulemavu ikiwemo programu ya mfuko wa jenga na Samia ambao umeanzishwa kwa ajili ya kusaidia makundi mbalimbali, ikiwemo ya Wenye Ulemavu”
Ameongeza kuwa Jamii hiyo inamshukuru sana Rais Dkt. Samia kwa namna alivyojenga ujumuishi kwa makundi ya watu wenye Ulemavu “Tumeshuhudia Serikali ya awamu ya Sita imekuwa Ni Serikali jumuishi, fedha ambazo zimepelekwa kwa watu wenye ulemavu zimewanufaisha sana, Tunajivunia na tunamuombea sana Mheshimiwa Rais”
Awali, Katibu Mkuu, Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu na Jonas Lubago amesema kuwa vyama vyote ambavyo chini ya SHIVYAWATA vinafurahia ruzuku inayotolewa na Serikali ya awamu ya sita. “Tumeshuhudia mikopo imekuwa ikitolewa kwa ile asilimia mbili ya Watu wenye ulemavu, tumeshuhudia watu wenye ulemavu wakipata ajira Serikalini na kupewa kipaumbele, mioyo yetu imeibeba awamu ya sita”
Ameongeza kuwa kipindi hiki cha awamu ya sita, Watu wenye Ulemavu tumenufaika kwa kuona wenzetu pia wameendelea kuhudumu katika nafasi mbalimbali za juu za uongozi Serikalini. “Katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na mageuzi makubwa ya Kimfumo ambayo imewezaha kuwa na utambuzi wa idadi ya watu wenye ualbino utakaosaidia utoaji huduma kwa wenye ualbino “