NA FAUZIA MUSSA
MKURUNGEZI Mtendaji Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Kenneth Simbaya amesema katika kipindi cha uchaguzi, nafasi ya waandishi wa habari ni ya muhimu sana katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, kwa wakati na kwa njia inayozingatia maadili ya uandishi wa habari.
Aliasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu kupambana na upotoshaji, taarifa za uongo na habari feki wakati wa uchaguzi yaliofanyika katika ukumbi wa kituo cha huduma za sheria (ZLSC) Kijangwani mjini unguja.
Alisema uzoefu unaonesha kuwa kipindi hicho huambatana na ongezeko la upotoshaji wa taarifa, taarifa za uongo zinazokusudiwa kupotosha pamoja na kusambaa kwa habari feki, ambazo zinaweza kuleta athari kwa jamii na kuvuruga amani.
“uzoefu unaonesha kuwa kutokana na kupanuka na kukua kwa teknolojia kumekuwa na ongezeko la habari feki ambapo waandishi wanapaswa kuwa makini kutokuingia katika mtego huo na badala yake kuwa msaada kwa jamii kuwapembulia habari sahihi.”alisema
Alieleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuimarisha maadili ya uandishi wa habari na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa kupambana na taarifa potofu na habari za uongo, hasa wakati wa uchaguzi mkuu 2025.
Alisema jamii inaanzisha mijadala mingi baada ya taarifa zinazotolewa kupitia vyombo vya habari vya kitaifa au mitandaoni na kuwasisitiza waandishi wa habari kuweka ajenda asilia hasa katika mitandao ya kijamii ili kuweka mijadala sahihi miongoni mwa watu.
Mapema aliwataka kuyatumia vyema mafunzo hayo yanayohusu mbinu za kisasa za kuthibitisha ukweli wa taarifa kwa kutumia teknolojia ikiwemo ya akaili unde ili kuwa na usahihi wa taarifa zao kabla ya kuzichapisha au kuzisambaza.
” Mkipata mkanganyiko kwenye taarifa Fulani mnaweza kutumia teknolojia mpya kama AI katika kujiridhisha usahihi wa taarifa zinazotolewa hasa kwenye mitandao ya kijamii.” Alisema
Alifahamisha kuwa mafunzo hayo yatakuwa endelevu ili kuwajengea uwezo waandishi chipukizi kuwa mabalozi wa taarifa sahihi na kuijengea uelewa jamii inayowazunguka.
Akiwasilisha mada Klkatika mafunzo hayo Ephraim Frem aliwasisitiza waandishi kuhakiki taarifa zao kabla ya kusambaza ili kuepuka kutoa taarifa za uongo zinazotolewa kwa makusudi ili kudhuru au kudanganya.
“Wakati mwengine taarifa hizo hutolewa bila nia mbaya iIi kuwa salama ni lazima tuzifuatilie kupitia teknolojia mbalimbali kama AI ambazo zinatumika kupata usahihi wa taarifa hizo” alisema
Alieleza kuwa baadhi ya wakati waandishi wanatumia taarifa sahihi zinazotumiwa nje ya muktadha bila kujua na hivyo kuwa sehemu ya kudhuru au kumshusha hadhi ya mtu.
Akifunga Mafunzo hayo Mwenyekiti WA Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Abdalla Abdul Rahman Mfaume, aliishukuru UTPC Kwa mafunzo hayo na kuahidi kuendelea kuwasimamia waandishi wa Klabu hizo katika kutatekeleza Kwa vitendo na kufikia malengo.
Alieleza kuwa katika ukuaji wa teknolojia ya habari upotoshaji umeongezeka na kusema kuwa waandishi wanapaswa kuhakikisha jamii inaendelea kupata habari sahihi wakati wote.
Aliwataka waandishi kutumia mafunzo hayo kwa vitendo na kuwa mabalozi wazuri Kwa Jamii kuweza kuishirikisha katika kutambua habari sahihi.
Waandishi wa habari washiriki walishukuru Kwa Mafunzo hayo wakitaja yamewajengea uwezo wa kutambua na kuchambua aina tofauti za taarifa potofu na habari feki.
Walisema kupitia mafunzo hayo wanatarajiwa kuwa mstari wa mbele katika kulinda ukweli na kusaidia kujenga jamii yenye kupambana taarifa sahihi na feki.
Takribani waandishi 20 Vijana kutoka Klabu ya waandishi wa habari Zanzibar walipata Mafunzo hayo wakitarajiwa kuendana na Kasi ya teknolojia ya habari na Mapinduzi ya kidigitali yanayoshuhudiwa ulimwenguni