
Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma limethibitisha kumpata Padre Camillus Nikata, wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) – Mwanza, baada ya kuripotiwa kupotea tangu Oktoba 9, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco G. Chilya, amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa Padre huyo hakutekwa kama ilivyodhaniwa awali, bali alijipoteza mwenyewe kutokana na changamoto za msongo wa mawazo.
“Tunaeleza kwa furaha kwamba Padre Camillus Nikata amepatikana akiwa hai. Taarifa zinaonesha kuwa alijipoteza kutokana na msongo wa mawazo na si tukio la utekaji kama ilivyoripotiwa,” amesema Kamanda Chilya.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Padre huyo alipatikana katika mashamba ya Kijiji cha Mawa, Kata ya Hanga, Wilaya ya Namtumbo eneo ambalo ni nyumbani kwao.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa alipokutwa, alikuwa amedhoofika kutokana na njaa, huku akiwa na begi dogo la mgongoni lenye vitu kadhaa.
Kamanda Chilya amesema Padre huyo kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songea (Homso) kwa ajili ya uchunguzi na matibabu baada ya kudhoofika kiafya.