Waziri mstaafu wa Maliasili na Utalii akizungumza na viongozi wa dini mkoani Mara.
Viongozi wa dini mkoani mara wakiwa kwenye kikao.
………..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Waziri Mstaafu wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu amekutana na viongozi wa dini Mkoani Mara kwa lengo la kuendelea kuzungumza nao ili wawahamasishe waumini wao suala la amani pamoja na kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Nyarandu amekutana na viongozi hao Oktoba 17, 2025 ikiwa ni muendelezo wake wa kukutana na makundi mbalimbali katika mikoa ya Kanda ya ziwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa dini wameisisitiza jamii kuendelea kuitunza amani hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi sanjari na kujitokeza kupiga kura ili waweze kuwachagua viongozi watakao wapatia maendeleo kwakipindi cha miaka mitano ijayo.
“Kumekuwepo na watu ambao wanatengeneza taharuki kwa wananchi juu ya zoezi la uchaguzi,hivyo Serikali inawajibu wa kuzuia na kuwakinda wananchi wake dhidi ya vitendo hivyo”, wamesema viongozi wa dini
Wamesema kuwa Amani ni Tunu pekee tuliyopewa na Mwenyezi Mungu hivyo watanzania wanapaswa walitambue hilo na waendelee kuilinda na kuitunza kwaajili ya maslahi mapana ya Taifa letu.
Kwaupande wake Mkuu wa mkoa wa Mara,Canal Evance Mtambi amesema majukumu ya vyombo vya ulinzi na usalama ni kulinda raia na mali zao.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kutojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani na badala yake washikamane katika hali ya umoja wakati na baada ya uchagizi mkuu.
Awali akielezea umuhimu wa kutunza amani Nyalandu amesema msingi wa umoja na mshikamano wa taifa ni pamoja na jamii kuishi kwa umoja huku akiwaasa viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa waumini juu ya umuhimu wa kuitunza amani na kupiga kura.