Na Neema Mtuka – Sumbawanga
Rukwa. Mgombea ubunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini, Aesh Halfan Hilary, amesema kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweza kuimarisha uchumi tangu alivyoingia madarakani, na kwa sasa Tanzania ina akiba ya dola za Marekani bilioni 6.7, sawa na shilingi trilioni 16.
Aesh Halfan ameyasema hayo leo Oktoba 19, 2025, katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Kizwite.
Amesema kuwa kwa Mkoa wa Rukwa kuna miradi mingi ya maendeleo ambayo wananchi wanajivunia, ikiwemo uwanja wa ndege, Chuo cha VETA, na hospitali ya Manispaa ya Sumbawanga.
Miradi mingine ni pamoja na Chuo cha Ualimu Sumbawanga kilichogharimu shilingi bilioni 4.8, mradi wa uboreshaji miji (TACTICS) wenye thamani ya shilingi bilioni 27.6, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga shilingi bilioni 61.1, na ujenzi wa Hospitali ya Manispaa pamoja na vifaa tiba kwa gharama ya shilingi bilioni 4.9.
Pia, Aesh amesema kuwa Dkt. Samia katika kipindi cha siku 100 atatoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwakopesha wanawake na vijana ili kujikwamua kiuchumi.
Aidha, amemshukuru mgombea urais huyo kwa kutoa fedha za ujenzi wa soko la mazao la kimataifa, ambalo litawasaidia wakulima kuuza mazao yao kwa uhakika.
Nao baadhi ya wananchi, akiwemo Agnes Mustapha kutoka Mtaa wa Katusa, wamewataka wagombea wote kutekeleza ahadi wanazozitoa ili kujenga imani kwa chama na serikali.
“Ninawaomba wagombea wote wa urais, ubunge na udiwani kuwa watekelezaji wa ahadi, maana tumezoea kuona ahadi hewa ambazo hazitekelezeki,” amesema Mustapha.
Naye kijana Ibrahim Ngulu amewaomba wagombea kuhakikisha wanasimamia utoaji wa mikopo kwenye halmashauri ili vijana wengi wanufaike na mikopo hiyo.
“Mikopo imekuwa na michakato mingi sana. Ikiwezekana ipunguzwe ili vijana tuipate na kuweza kufanya biashara mbalimbali zitakazotuingizia kipato,” amesema Ngulu.