
Dar es Salaam, Oktoba 20, 2025 — Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amemkabidhi rasmi hati ya nyumba Mjane wa marehemu Justus Rugaibula, Bi Alice Nyamwiza Haule, iliyopo eneo la Msasani Beach, Kiwanja Na. 819, baada ya tume maalum aliyoiunda kupitia malalamiko yake kutoa majibu na kuthibitisha kuwa mjane huyo alikuwa akidhulumiwa.
Bi Alice, ambaye ni msimamizi wa mirathi ya marehemu mumewe, amekabidhiwa hati hiyo leo ikiwa ni ishara ya kurejesha haki yake baada ya kupitia kipindi kigumu cha kudhalilishwa na kutishiwa kutolewa kwa nguvu katika nyumba hiyo na mtu anayedaiwa kuwa ‘kigogo’ aitwaye Bwana Mohammed. Tukio hilo lilizua taharuki kubwa mitandaoni baada ya video zake kusambaa zikionesha manyanyaso aliyokuwa akipitia.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, RC Chalamila alisema Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam haitavumilia vitendo vya dhuluma, hasa vinavyowalenga wajane, watoto, na makundi yenye uhitaji maalum.
“Haki ni ya kila mtu, na Serikali itahakikisha kila mwananchi anapata stahiki zake kwa mujibu wa sheria. Hatutavumilia watu wanaotumia nafasi au majina makubwa kudhulumu wanyonge,” alisema Chalamila.
Mbali na kukabidhi hati hiyo, RC Chalamila pia alimkabidhi Bi Alice kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuanzisha maisha mapya baada ya kipindi kigumu alichopitia. Alisema msaada huo ni sehemu ya kuonyesha mshikamano wa kijamii na kuthamini utu wa binadamu.
Bi Alice, akizungumza kwa hisia, alimshukuru Mkuu wa Mkoa na Serikali kwa kusimama upande wa haki, akisema alikata tamaa kutokana na hofu na vitisho alivyopata, lakini sasa amepata faraja kubwa.
“Sikuamini kama haki ingeweza kutendeka. Namshukuru Mungu na Serikali kwa kusikia kilio changu. Leo nimepumua,” alisema kwa machozi ya furaha.
Tukio hilo limepokelewa kwa pongezi nyingi kutoka kwa wakazi wa Dar es Salaam na watumiaji wa mitandao ya kijamii, wakimpongeza RC Chalamila kwa kusimamia haki na kutoa mfano wa uongozi wa karibu na wananchi.