Na Yohana Kidaga- Rufiji
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan
amewaomba wananchi wa jimbo la Rufiji kumpa kura za ushindi Mgombea wa jimbo hilo Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa kuwa ni mtu mwenye uwezo na tayari ameonyesha uwezo mkubwa katika Wizara nne alizomteua kuzisimamia.
Mhe. Mchengerwa ni miongoni mwa viongozi waandamizi wachache hapa nchini ambao wamepata bahati ya kuhudumu kwenye mihimili yote katika nafasi za juu.
Mgombea huyo wa Urais amesema haya leo Oktoba 20, 2025 kwenye mkutano wa kampeni zake alioufanya Ikwiriri- Rufiji ambapo amewasihi wamchague Mchengerwa a.k.a MTU KAZI ili aendelee kuwafanyia kazi hatimaye kuwaletea maendeleo.
“Ndugu zangu tunaposema kazi na utu tunasonga mbele tunamaanisha kuwa tunapoleta maendeleo na kuyaboresha maisha ya watanzania kwa kuboresha huduma za jamii ndiyo tunaboresha utu wao”. Amefafanua Mhe. Samia huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliofurika kwenye uwanjaa wa ujamaa Ikwiriri wilayani Rufiji
Aidha amesisitiza kuwa Mchengerwa ni kiongozi makini, mchapakazi na mwenye maono ya kuleta mageuzi chanya katika maendeleo ya Rufiji.
Dkt. Samia amewaeleza wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka msingi imara wa maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati, hivyo ni muhimu kuendelea kuwa na viongozi wanaoendana na kasi ya utekelezaji na wanaoweza kusimamia ajenda za maendeleo kwa vitendo.
Kwa upande wake mgombea wa nafasi ya Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Mchengerwa amempongeza na kumshukuru Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan kwa mapinduzi makubwa aliyoyafanya kwenye sekta mbalimbali hapa nchini.

Akitolea mfano amesema kiasi cha zaidi ya shilingi trilioni 1.56 kilichotolewa kwa ajili ya elimu bure kimekuwa mkombozi mkubwa kwa wazazi, walezi, akina mama na wazee kote nchini, ambao sasa wana uhakika wa kuwaona watoto wao wakisoma bila mzigo wa ada.
“Wazee wa Rufiji, wazazi na walezi wote, tunasema asante. Umewapunguzia mzigo mkubwa Watanzania. Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Pwani, nakushukuru sana sana Dkt. Samia. Umeandika ukurasa mpya wa matumaini katika sekta ya elimu,” amesema Mchengerwa.

Mkutano huo uliojaza maelfu ya wananchi ulitumbuizwa na wasanii mbalimbali wa muziki na wasanii wa sanaa za maigizo.


