
Katika kuendelea kuhamasisha uwekezaji na kuimarisha ushirikiano na Watanzania wanaoishi nje ya nchi, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kwa kushirikiana na Benki ya TCB na Ubalozi wa Tanzania nchini Canada wamefanya makongamano ya uwekezaji katika miji ya Toronto na Calgary.
Makongamano hayo yalilenga kuwapatia wanadiaspora elimu kuhusu Fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania,Huduma za kifedha zinazotolewa na Benki ya TCB kwa wawekezaji naUshirikiano wa biashara na miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini.
Katika mijadala hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Bw. Gilead Teri, alisisitiza dhamira ya Serikali kuhakikisha Watanzania wanaoishi nje wanashiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa taifa kupitia uwekezaji endelevu.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Canada, Mhe. Joseph Sokoine, alitoa shukrani kwa TISEZA na TCB kwa juhudi walizofanya, na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuwahamasisha Watanzania waishio nje ya nchi kushiriki katika uwekezaji kama njia ya kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Naye Bi Lilian Mtali Mkurugenzi wa Biashara kutoka Benki ya TCB, alieleza huduma maalum zinazotolewa kwa diaspora, ikiwemo akaunti za uwekezaji, mikopo, na huduma za kidigitali zinazowezesha miamala ya kifedha kufanyika kwa urahisi kutoka nje ya nchi.
Makongamano haya yalipata mwitikio mkubwa kutoka kwa Watanzania waishio Canada, wakionesha hamasa kubwa ya kushirikiana na taasisi za Tanzania katika kukuza uchumi. Viongozi wa Jumuiya ya Watanzania waishio Canada walieleza kuwa wamefaidika sana na elimu hiyo na wamepanga kutumia fursa zilizopo kuhakikisha Watanzania wanawekeza nyumbani.