

Watu wasiopungua 14 wamefariki dunia na wengine 29 kujeruhiwa baada ya treni ya abiria kupata ajali mashariki mwa Ethiopia, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa Jumanne na vyombo vya habari vya serikali.
Taarifa ya Dire TV, chombo cha habari cha serikali, imeeleza kuwa ajali hiyo ilitokea majira ya saa nane usiku wakati treni hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka mji wa Dewele, ulioko karibu na mpaka wa Djibouti, kuelekea Dire Dawa umbali wa takribani kilomita 200.
“Ajali iliyotokea katika reli ya Dire Dawa Dewele imewaua watu 14 na kujeruhi wengine 29, baadhi yao wakiwa na majeraha makubwa,” ilisomeka taarifa ya kituo hicho katika ukurasa wake wa Facebook.
Picha zilizochapishwa na vyombo vya habari vya ndani zilionyesha mabehewa kadhaa yakiwa yamepinduka na mengine yakiwa yamevunjika vibaya, zikionesha ukubwa wa maafa hayo.
Maafisa wa eneo hilo hawajatoa maelezo ya kina kuhusu chanzo cha ajali, ingawa mamlaka za usafiri nchini humo zimeanza uchunguzi ili kubaini kilichosababisha tukio hilo.
Ajali za treni si za kawaida nchini Ethiopia, taifa lenye idadi ya watu takriban milioni 130, ambalo linashikilia nafasi ya pili kwa wingi wa watu barani Afrika baada ya Nigeria.
Ajali kubwa zaidi ya reli kuwahi kuripotiwa nchini humo ilitokea mwaka 1985, ambapo zaidi ya watu 400 walipoteza maisha na wengine 500 kujeruhiwa, baada ya treni iliyokuwa ikitokea Djibouti kuelekea Addis Ababa kuanguka kwenye korongo.
ALLY KAMWE FUNGUKA KUHUSU KOCHA MPYA – KUFUNGWA MALAWI – MECHI YA MARUDIANO…









