NA DENIS MLOWE, IRINGA
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Ngajilo amewaahidi wakazi wa Igumbilo tawi la Ulonge atahakikisha anapambana kata hiyo ipate gari la kubebea wagonjwa endapo watampa kura katika uchaguzi wa Oktoba 29 mwaka huu.
Ngajilo aliyasema hayo katika mkutano wa kampeni wa chama hicho katika tawi la Ulonge katika kata ya Igumbilo akizungumza na mamia ya wananchi waliojitokeza katika mkutano akiomba kura kwa ajili ya mgombea urais Dk. Samia Suluhu Hassan na Diwani wa kata hiyo Jackson Chatanda.
Alisema kuwa wamejipanga pamoja na mgombea udiwani kuhakikisha kwamba kituo cha afya kinajengwa kwenye kata hiyo na kutokana na kuwa nje kidogo ya mji watahakikisha wanapata gari la kubebea wagonjwa ili kutoa huduma kwa wananchi.
“Changamoto za kata ya Igumbilo tutashirikiana kwa nguvu zote katika kuleta maendeleo na kituo cha afya kinajengwa tutasimamia vyema ili kiweze kufanya kazi vyema na kutoa huduma za kijamii zinazotakiwa kutolewa za elimu na afya huduma nyingi lazima zije Igumbilo kutokana na huku ju pembezoni” Alisema.
Alisema kuwa atahakikisha Kituo cha afya kiwe na huduma nyingi kwa ajili ya wananchi na gari la kubeba wagonjwa litawasaidia sana kwa wakazi mtaa wa uwongouwongo na Matungulu.
Akizungumzia maendeleo yaliyoletwa na Rais Samia, Ngajilo amesema ushuhuda wa mirasi aliyosambaa kila kona ya Tanzania ni kielelezo tosha cha uongozi bora wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na hivyo anastahili kuitwa shujaa wa maendeleo wa taifa.
“Kila kona ya nchi yetu leo kuna miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya watu barabara, shule, zahanati, hospitali, maji na umeme yote haya ni matokeo ya dira ya uongozi wa Dkt. Samia. Ni shujaa wa maendeleo na tunapaswa kumheshimu kwa kumrejesha madarakani kwa kura nyingi,” alisema
Ngajilo pia amewahimiza wananchi wa Iringa kuendelea kuunga mkono wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais, akisisitiza kuwa chama hicho kimejipambanua kwa vitendo, si kwa maneno.
Aliongeza kuwa Ulonge kuna changamoto ya umeme na maji na eneo la Matungulu hivyo kuhakikisha wanapata maji na umeme kwani yamepita na maji yanatakiwa kuyapelekwa kwa wananchi ni suala la kuwafata iruwasa na TANESCO.