Na Mwandishi Wetu WMJJWM- Mbeya
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mbeya kufanya kazi kwa bidii na kujituma katika kuwahudumia wananchi katika vituo vyao vya kazi.
Mdemu ameyasema hayo leo tarehe 22 Oktoba, 2025, wakati akikabidhi Pikipiki kumi na mbili (12) kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii katika hafla fupi iliyofanyika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya lengo kuu ikiwa ni kuwasaidia Maafisa hao hasa wanaoishi vijijini kuzitumia kuwafikia wananchi na kuwahudumia kwa wakati.
Mdemu amesema lengo kuu la kuwapatia pikipiki hizo ni kutambua thamani ya mchango wao kiutendaji pamoja na kuwarahisishia kazi wakati wa ufuatiliaji na utatuzi wa changamoto za kijamii.
“Tunaomba mkawajibike ipasavyo kwani kwa sasa mmerahisishiwa utendaji kazi wenu kwa kupewa vyombo vya usafiri (Pikipiki) ili kuwafikia wananchi katika maeneo yao na kuwahudumia.” amesema Mdemu.
Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya Anna Mwambene ameishukuru Wizara kwa kuwapatia Maafisa hao vyombo vya usafiri hivyo ambavyo anaamini vitaleta chachu na mabadiliko katika kuwahudumia wananchi mkoani humo.
“Mmekabidhiwa pikipiki hizi mzitunze ili zifanye kazi ilivyokusudiwa na niiombe Wizara kuendelea kusaidia vyombo vya usafiri kila wakati ili kukidhi mahitaji ya Maafisa Maendeleo ambao kazi zao zinawahitaji kusafiri umbali mrefu kuwafuata wananchi walipo.” amesema Anna
Aidha Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mbeya Elukaga Mwaikasu amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii Kata waliopewa vyombo vya usafiri (pikipiki) hivyo kuhakikisha wanavitunza na kwa yeyote atakayeharibu makusudi au kukitumia chombo ndivyo sivyo hatua za kisheria zitachuliwa dhidi yake.
Kwa upande wao Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata waliopokea vyombo vya usafiri (pikipiki) hivyo wameipongeza Serikali kwa kutoa vitendea kazi na kuahidi kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuwatumikia na kuwahudumia wananchi kwa weledi na kwa ufanisi.