
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, amekamatwa na maafisa wa Jeshi la Polisi leo Jumatano, Oktoba 22, 2025, akiwa katika viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam.
Taarifa hizo zimethibitishwa na Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa CHADEMA, Wakili Gaston Garubindi, ambaye amewaeleza wanahabari kwamba Heche amesafirishwa kuelekea Tarime, mkoani Mara, ambako inadaiwa ana kesi inayomkabili.
“Ni kweli, Makamu Mwenyekiti wetu John Heche amekamatwa leo asubuhi akiwa anaingia Mahakamani. Taarifa tulizopata ni kwamba anapelekwa Tarime kwa ajili ya kesi inayodaiwa kumkabili huko,” alisema Wakili Garubindi akiwa nje ya viwanja vya Mahakama Kuu.
Hadi kufikia muda huu, bado haijafahamika wazi aina ya kesi au tuhuma zinazomkabili mwanasiasa huyo, huku viongozi wa chama hicho wakieleza kuwa wanafuatilia kwa karibu mwenendo wa tukio hilo.
Tukio hili limezua taharuki miongoni mwa wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wakifuatilia shughuli za mahakamani, ambapo baadhi yao walionekana kuonyesha wasiwasi kuhusu usalama wa kiongozi wao.
Jeshi la Polisi halijatoa tamko rasmi hadi sasa kuhusu sababu kamili za kukamatwa kwa Heche wala utaratibu wa kisheria unaoendelea kufuatwa.