Na Mwandishi Wetu WMJJWM- Iringa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu amewataka Maofisa Maendeleo ya Jamii kutumia pikipiki walizopewa na Serikali kuwafikia wananchi vijijini na kuwahudumia kwa weledi.
Dkt. Jingu amesema hayo tarehe 22 Oktoba, 2025 wakati akikabidhi pikipiki kumi (10) kwa Maofisa Mendeleo ya Jamii Mkoani Iringa kwa lengo la kuboresha utendaji na kuwafikia wananchi katika maeneo yao.
“kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninafuraha kukabidhi jumla ya pikipiki kumi (10) kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Iringa. Pikipiki hizi ni sehemu ya pikipiki 98 zilizonunuliwa na Wizara kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi wa Maafisa wetu katika ngazi ya kata.” amesema Dkt. Jingu.
Ameongezea kuwa katika mgao huo, Halmashauri tano za Mkoa wa Iringa zimepokea pikipiki mbili (2) zikiwemo Mufindi DC, Mafinga TC, Iringa DC, Kilolo DC, na Iringa MC. Aidha, Chuo cha Maendeleo ya Jamii Rungemba na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha, kila kimoja kimepokea pikipiki moja (1) kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa programu za ushirikishwaji jamii na kuratibu Dawati la Jinsia katika maeneo Jirani.
“Mpaka sasa jumla ya pikipiki (110) tayari zimegawiwa kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini. Kati ya hizo; mwaka (2023), pikipiki Ishirini na Tano (25) Mwaka (2024), pikipiki Themanini na Tano (85) ziligawiwa mwezi Septemba. Pikipiki Tisini na Nane (98) mwaka huu na kufikisha jumla ya pikipiki Mia Mbili na Nane (208) hatua ambayo itaendelea kuimarisha uwezo wa Maafisa wetu katika kufikia jamii kwa ufanisi zaidi.” ameongezea Dkt. Jingu.
Ameeleza kuwa moja ya malengo ya Pikipiki hizo ni kusaidia katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kuhamasisha na Kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi (Bottom-Up) kwa kipindi cha mwaka 2022/23-2025/26. Mpango ambao ulianza kutekelezwa rasmi mwezi Februari 2023, unaolenga kuboresha mfumo wa utendaji kazi na utoaji huduma katika ngazi ya msingi kwa kuhakikisha kuwa watendaji wa Serikali wanawezeshwa kirasilimali ili waweze kuwafikia wananchi kikamilifu.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Doris Kalasa, amesema Pikipiki hizo zitasaidia na kurahiisisha utendaji wa maafisa maendeleo kwa kuwafikia wananchi kwa urahisi kwa kuboresha mawasiliano, usimamizi wa shughuli za maendeleo na uhamasishaji wa fursa za kiuchumi kama vile VICOBA na SACCOS.
Nao Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata waliopokea vyombo vya usafiri (pikipiki) hivyo wameipongeza Serikali kwa kutoa vitendea kazi na kuahidi kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuwatumikia na kuwahudumia wananchi kwa weledi na kwa ufanisi.