Na Meleka Kulwa – Dodoma
Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Profesa Hosen Mayaya, amesema kuwa Mradi wa HEET (Higher Education for Economic Transformation) unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ya juu nchini.
Ameyasema hayo Oktoba 24, 2025, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo chuoni hapo.
Prof. Mayaya amesema kuwa mradi wa HEET unatekelezwa katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi tano zilizo chini ya Wizara ya Fedha, ikiwemo IRDP.
Amesema kuwa Chuo cha Mipango kimetengewa jumla ya Dola za Kimarekani milioni 5.675, sawa na shilingi bilioni 13.9, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu, kuboresha mitaala, kuimarisha mbinu za ufundishaji, kuendeleza rasilimali watu, kukuza tafiti na ubunifu pamoja na kuimarisha elimu jumuishi na usawa wa kijinsia.
Aidha, amesema kuwa katika mradi huo litajengwa jengo la taaluma lenye ghorofa tano katika eneo la Miyuji, Kampasi Kuu Dodoma, ambalo litakuwa na kumbi za mihadhara, maabara za kompyuta, studio, ofisi na miundombinu rafiki kwa watu wenye mahitaji maalum.
Profesa Mayaya amesema kuwa katika jengo Hilo kumeongezwa gorofa ya Tano ambayo itajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 11, ikiwemo vifaa kama viti, meza, kompyuta na mtandao wa intaneti. Amebainisha kuwa litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,628 kwa wakati mmoja na litaboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Aidha, amesema kuwa mradi huo umechangia kutoa ajira kwa wananchi wa eneo husika na kuongeza kipato kwa wafanyabiashara wadogo ikiwemo mama lishe.
Prof. Mayaya amebainisha kuwa kupitia HEET, chuo kimefanya mapitio ya mitaala miwili ikiwemo Shahada ya Kwanza ya Usimamizi na Tathmini ya Ardhi (Land Management and Valuation) na Shahada ya Umahiri ya Mipango na Usimamizi (Planning and Management).
Amesema kuwa mitaala hiyo imeboreshwa kwa kushirikiana na tasnia husika ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi unaohitajika sokoni, na imezingatia masuala muhimu kama mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya nishati safi.
Aidha, amebainisha kuwa chuo kimewajengea uwezo wahadhiri 65 katika mbinu bunifu za ufundishaji na matumizi ya TEHAMA, huku watumishi 75 wakipatiwa mafunzo ya muda mfupi na mrefu. Kati yao, watumishi watatu wanasoma Shahada ya Uzamivu (PhD) ndani ya nchi na wawili nje ya nchi.
Prof. Mayaya amesema kuwa chuo kimefanya maboresho makubwa ya mifumo ya TEHAMA kwa kutandaza nyaya za faiba na kuongeza kasi ya mtandao wa intaneti kutoka MBps 20 hadi 307, huku matarajio yakiwa kufikia 1000 Mbps ifikapo mwaka 2026.
Aidha, amebainisha kuwa chuo kimeunda majukwaa ya kujifunzia na kufundishia kwa njia ya mtandao na kitaanza kutoa mafunzo ya muda mrefu kwa njia ya masafa kuanzia mwaka wa masomo 2025/26.
Pia, Prof. Mayaya amesema kuwa kupitia HEET, IRDP imeanzisha mfumo wa kisasa wa uchapishaji wa makala za kitaaluma unaopatikana mtandaoni kupitia tovuti ya chuo na mitandao ya kimataifa, hatua ambayo imeongeza ushirikiano wa kimataifa katika utafiti na machapisho.
Aidha, amesema kuwa chuo kimeunda Kamati ya Ushauri wa Tasnia (Industrial Advisory Committee) na kusaini mikataba 10 ya ushirikiano na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwemo Wizara ya Fedha, Tume ya Ushirika, African Peer Review Mechanism, UNCDF na Chuo Kikuu cha Eswatini.
Amesema kuwa kupitia mradi wa HEET, chuo pia kimeimarisha elimu jumuishi na usawa wa kijinsia kwa kuzingatia mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu katika mitaala, kutoa mafunzo ya kijinsia kwa wahadhiri na kuanzisha dawati la kijinsia linaloratibu masuala hayo chuoni.
Aidha, Prof. Mayaya amebainisha kuwa mradi wa HEET unachangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Ilani ya CCM ya 2025-2030 na Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 toleo la mwaka 2023, kwa kujenga rasilimali watu wenye ubunifu na ujuzi unaohitajika katika uchumi wa kisasa.
Amesema kuwa chuo kimepata manufaa makubwa kupitia mradi huo na kimeweka mikakati ya kuhakikisha uendelevu wake kwa kuingiza shughuli zilizotekelezwa na HEET katika mipango ya muda mfupi na mrefu pamoja na bajeti ya kila mwaka.
Aidha, amesema kuwa masuala hayo yataingizwa katika mpango mkakati mpya wa chuo utakaoanza kutekelezwa mwaka 2027, unaoendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Prof. Mayaya pia ametoa wito kwa jumuiya ya Chuo cha Mipango na Watanzania wote kujitokeza kuhakiki majina yao ya wapiga kura na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi.
Kwa upande wake Mkandarasi wa mradi huo, Mhandisi Joseph Akida, amesema utekelezaji wa miradi ya miundombinu na TEHAMA unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika kwa wakati kama ulivyopangwa, ili kuhakikisha malengo ya mradi yanatimia kikamilifu.








