Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa kufunga kambi maalumu ya upasuaji wa moyo iliyofanywa na wataalam wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Open Heart International (OHI) la nchini Australia ambapo wagonjwa 17 wamefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo.
Picha 2: Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo wa Shirika la Open Heart International (OHI) la nchini Australia Darren Wolfers akielezea ushirikiano uliopo kati ya shirika hilo na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kufunga kambi ya upasuaji wa moyo uliyomalizika leo jijini Dar es Salaam. Jumla ya wagonjwa 17 wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi hiyo.
Picha 3: Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya akitoa neno la shukrani wakati wa kufunga kambi maalumu ya upasuaji wa moyo iliyofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Open Heart International (OHI) la nchini Australia. Jumla ya wagonjwa 17 wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi hiyo.
Picha 4: Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpatia tuzo ya Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka Shirika la Open Heart International (OHI) la nchini Australia Darren Wolfers wakati wa hafla fupi ya kufunga kambi maalumu ya upasuaji wa moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalam wa JKCI na OHI leo jijini Dar es Salaam. Jumla ya wagonjwa 17 wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi hiyo. (Picha na JKCI)
…………
Na Mwandishi Maalumu -Dar es Salaam
24/10/2025 Serikali kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa zaidi ya shilingi milioni 500 ambazo zingetumika kugharamia matibabu ya wagonjwa 17 waliofanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu, endapo wangepelekwa kutibiwa nje ya nchi.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa kufunga kambi hiyo ya siku tano iliyofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Open Heart International (OHI) la nchini Australia.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba alisema upasuaji huo wa kufungua kifua umefanyika kwa wagonjwa 17 watu wazima wanne na watoto 13.
“Hii ni mara ya 14 kwa timu ya watalaamu kutoka Shirika la Open Heart International kuja katika Taasisi yetu kusaidia kutoa huduma za upasuaji wa moyo, wameshatoa matibabu kwa zaidi ya wagonjwa 200 na hivyo kuokoa maisha yao”, alisema. Dkt Kisenge.
Aidha Dkt. Kisenge aliwapongeza wataalamu hao kwa kutoa mafunzo ya teknologia ya vifaa tiba kwa wahudumu wa afya wa JKCI wakiwemo madaktari wa upasuaji, wauguzi na wataalamu wa vifaa tiba mafunzo hayo yataendelea kuifanya Taasisi hiyo kuwa kinara wa utoaji wa huduma bora za moyo.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa Shirika la Open Heart International la nchini Australia (OHI) ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo Darren Wolfers alisema wanajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya JKCI tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015.
“Tunakuja kila mwaka kutoa matibabu ya kuokoa maisha ya watoto na watu wazima nchini Tanzania kwa sababu kuna wagonjwa wengi wenye matatizo ya moyo wanaohitaji kupata huduma za matibabu ya kibingwa”, alisema Dkt. Wolfers.
Nao wagonjwa waliopata matibabu katika kambi hiyo waliishukuru serikali ya awamu wa sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za matibabu ya moyo nchini hii ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu na kununua vifaa tiba vya kisasa.
“Ninawashukuru wataalamu wa afya wa JKCI na wenzao kutoka nje ya nchi ambao wamenifanyia upasuaji wa moyo wamenipa huduma nzuri, ninawaomba wenzangu wanaosumbuliwa na maradhi ya moyo na hawana uwezo wa kulipia matibabu wasikate tamaa waje kupata huduma kwani hata mimi sikuwa na uwezo kifedha na nimehudumiwa”, alisema Efigenia Kowi.
“Mwanangu aligundulika kuwa na shida ya moyo mara baada ya kuzaliwa, ninawashukuru wataalamu hawa wamemfanyia upasuaji siku ya Jumatatu na anaendelea vizuri. Ninawaomba watanzania wenzangu wasihangaike kwenda nje ya nchi kufuata huduma za matibabu ya moyo kwani matibabu mazuri ya moyo ya kiwango cha kimataifa yanapatikana hapa nchini”, alisema Jumaa Salum.








