Kaimu Msajili wa Hazina, Bi. Lightines Mauki akizungumza na waandishi wa habari leo, tarehe 27 Oktoba 2025, jijini Dar es Salaam.
………
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imewakumbusha na kuwasisitiza watumishi wote wa umma waliopo katika taasisi na mashirika ya umma kote nchini kutumia haki yao ya msingi ya kikatiba kwa kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.
Aidha, Ofisi hiyo imetoa wito kwa wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kuhakikisha kuwa watumishi wao wanapatiwa fursa ya kutekeleza haki hiyo, muhimu bila kuathiri majukumu yao ya kikazi, kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Msajili wa Hazina, Bi. Lightines Mauki, wakati akizungumza na waandishi wa habari leo, tarehe 27 Oktoba 2025, jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa pamoja na majukumu hayo, Ofisi pia inahakikisha usimamizi bora na ustawi wa rasilimali watu waliopo katika taasisi hizo, ili kuimarisha uwajibikaji, uadilifu, na mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
“Katika kuzingatia majukumu hayo, Ofisi inawakumbusha watumishi wote katika taasisi na mashirika ya umma kwamba kushiriki uchaguzi ni wajibu wa kiraia unaojenga demokrasia, umoja, na uthabiti wa Taifa,” amesema Bi. Mauki.
Ameongeza kuwa kupiga kura ni chombo cha mabadiliko chanya kinachowawezesha wananchi kuchagua viongozi wenye maono, uadilifu na uwajibikaji.
Aidha, amesisitiza kuwa ushiriki mkubwa wa watumishi wa umma unaonesha mfano wa uzalendo, nidhamu ya kitaifa, na uelewa wa majukumu ya kikatiba.
Amefafanua kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina inaamini kwamba, kwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huu, watumishi wa umma wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha utawala bora, uchumi endelevu na ustawi wa wananchi.
Ofisi ya Msajili wa Hazina ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina (Madaraka na Majukumu), Sura ya 370, na ina jukumu la kusimamia na kuendeleza uwekezaji wa Serikali katika taasisi na mashirika ya umma, pamoja na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi.






