

Washington, Marekani — Zaidi ya safari 1,400 za ndege zimefutwa nchini Marekani Jumamosi hii, huku takribani safari 6,000 nyingine zikiahirishwa, kufuatia hatua ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (FAA) kupunguza shughuli zake katika viwanja vikubwa vya ndege kutokana na athari za kufungwa kwa serikali ya Marekani (government shutdown).
Kwa mujibu wa tovuti ya FlightAware, ambayo hufuatilia safari za ndege duniani, idadi hiyo ya kufutwa na kuchelewa kwa safari imeathiri abiria maelfu kote nchini, huku hali ikitarajiwa kuendelea kuwa ngumu endapo mgogoro wa kisiasa utaendelea.

FAA ilitangaza mapema wiki hii kuwa itapunguza hadi asilimia 10 ya shughuli za safari za anga katika viwanja 40 vya ndege vyenye shughuli nyingi zaidi nchini humo. Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia uchovu unaoripotiwa miongoni mwa wadhibiti wa safari za anga (air traffic controllers) ambao wamekuwa wakifanya kazi bila malipo tangu kufungwa kwa serikali kuanza Oktoba 1.
Hali hii imezidisha msongo na usumbufu kwa mashirika ya ndege na abiria, huku baadhi ya mashirika yakilazimika kubadilisha ratiba au kufuta safari kabisa.
Kwa upande wa kisiasa, Warepublican na Wademokrat bado wamegawanyika kuhusu jinsi ya kumaliza mkwamo wa bajeti uliosababisha serikali kufungwa. Mazungumzo ya kusaka suluhu yanaendelea, lakini mpaka sasa hakuna makubaliano yaliyofikiwa.
Kufungwa huku kwa serikali kumeathiri sekta kadhaa muhimu ikiwemo usafiri wa anga, huduma za jamii na taasisi za serikali, huku wananchi wengi wakihofia madhara zaidi endapo hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu.
KWA MARA ya KWANZA MAKAMU NCHIMBI AZUNGUMZIA VURUGU za UCHAGUZI – “NCHI YETU ni SALAMA”…






