Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa :Watu 10 wakazi wa Sumbawanga mkoani Rukwa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga kwa kosa la uhaini na kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, makosa ambayo wanatuhumiwa kuyafanya kati ya mwezi Machi mpaka Oktoba 30, 2025.
Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa serikali David Mwakibolwa amesema watuhumiwa hao ni Grace Sixto Mafuta (42), Samson Baruti Noel (25), Isack Melimeli Myamba (24), Frank Charles Nyansio (42), Filbert Jolam Malela (29), Erenest Ernest Kanoni (24), Meshack Charles Mwambinga (25), Alfred Jastine Bendera (22), Boniface Richard Kalezu (30) na Daud Evod Machelela (22).
Washitakiwa hao wamepandishwa kizimbani leo Novemba 11, 2025 na kusomewa mashitaka mawili ya kesi namba PI 16146 /2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga Mh.Kisasila Saguda.
Akisoma mashitaka hayo Wakili wa Serikali David Mwakibolwa amesema kosa la kwanza ni kuwa kwa nyakati tofauti ya mwezi Machi mpaka Oktoba 30, 2025 katika maeneo tofauti ndani ya mkoa wa Rukwa walikula njama na kutenda kosa la Uhaini chini ya kifungu cha sheria namba 384 cha mwenendo wa makosa ya jinai marejeo ya kifungu cha 16 cha mwaka 2023.
Katika kosa la Pili, Wakili wa Serikali amesema washitakiwa hao walitenda kosa la uhaini chini ya kifungu cha 39 (2)(d)cha pili cha sheria ya kanuni ya adhabu, sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023, ambapo maelezo ya kosa ni kuwa washitakiwa mnamo tarehe 30 ya mwezi wa kumi mwaka 2025 katika mji wa Sumbawanga walikuwa na nia ya kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kuitishia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kujiingiza kufanya fujo na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za serikali zinazotumika kutolea huduma muhimu.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga, Mh. Kisasila Saguda amewataka washitakiwa hao kutojibu chochote hadi hapo shauri hilo litakapokwenda kusikilizwa kwenye Mahakama Kuu.
Upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika kwa makosa hayo mawili na kwamba makosa yote hayana dhamana na washitakiwa wamerudishwa mahabusu hadi tarehe 24 mwezi wa Kumi na Moja mwaka 2025 kesi itakapo tajwa tena.






