

Mchezaji wa Klabu ya Yanga SC, Aziz Andabwile ameweka wazi ukweli kuhusu taarifa zilizokuwa zikisambaa mitandaoni zikimhusu yeye na Klabu hiyo.
Kupitia taarifa yake kwa umma, mchezaji huyo amesema kuwa bado ni mchezaji halali wa Yanga SC na kwamba haki zake zote za kimkataba tayari zimeshalipwa na Klabu.
“Mimi ni mchezaji wa Young Africans Sports Club na haki zangu za kimkataba tayari nilishalipwa,” amesema.
Aidha, amewaomba waandishi wa habari kuhakikisha wanakuwa na vyanzo sahihi vya taarifa kabla ya kuchapisha habari, ili kuepuka kuleta taharuki miongoni mwa wachezaji na ndani ya timu zao.
“Niwaombe ndugu waandishi wa Habari kuwa na vyanzo sahihi vya taarifa ili kutoleta taharuki kwa wachezaji kwenye timu zao,” ameongeza.
Mwisho, ameomba radhi kwa wote waliochanganyikiwa au kukwazika kutokana na sintofahamu iliyojitokeza mitandaoni, huku akisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuitumikia Klabu ya Yanga kwa uaminifu na kujituma.






