Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
MKOA wa Ruvuma,umefanya mnada wa kwanza wa zao la korosho katika msimu 2025/2026 ambapo jumla ya kilo milioni 6.3 zimeuzwa huku bei wastani ikiwa Sh.3,281 kwa kilo moja.
Akizindua mnada huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Katibu Tawala wa Wilaya ya Tunduru Milongo Sanga,amewataka wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo,kutumia mbegu bora na pembejeo ambazo zitachangia kuzalisha korosho bora na kulinda soko la zao hilo.
Abbas amesema,lengo la Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Kilimo ni kuhakikisha nchi yetu inazalisha korosho zenye ubora zitakazowavutia wanunuzi wa ndani na nje ya Tanzania.
Amesema,Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itaendelea kuchukua hatua kudhibiti uingizaji wa mbegu feki na kuwachukulia hatua kali watu watakaojaribu kuingiza mbegu zisizofaa sokoni.
Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa moyo wa kizalendo na dhamira ya dhati katika kuboresha huduma za kilimo kwenye zao la korosho kwani katika kipindi chake zao la korosho limekuwa kwa kasi kubwa ikiwemo kupanda kwa bei ya zao hilo.
“Mathalani mwaka 2023/2024 bei ya korosho kwa kilo ilikuwa Sh.7,100 wakati mwaka 2024/2025 bei ilikuwa Sh.2,942,hakuna hofu kwamba katika kipindi kingine cha uongozi wake 2025 hadi 2030 zao la korosho litazidi kuimarika”amesema Abbas.
Amewataka wakulima kutumia mvua za mwanzo wa msimu kupanda mazao na kutumia njia bora ya kuhifadhi mazao kwa kuepuka kuhifadhi kwa kutumia viuatilifu au dawa za maji badala yake kutumia teknolojia inayozuia hewa kuingia kwenye mazao ikiwemo mifuko ya kinga njaa.
Amesema,Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaweka mazingira wezeshi na rafiki ya bei ya mazao ikiwemo zao la korosho linalolimwa kwa wingi katika Wilaya ya Tunduru.
Amewaomba wakulima na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kujenga Taifa lenye usalama,amani na maendeleo endelevu.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru(TAMCU LTD) Mussa Manjaule amesema, jumla ya kampuni 25 zilijitokeza kununua korosho kati ya hizo kampuni 16 zilishinda.
Manjaule,amewashukuru wakulima kwa kukubali kuuza korosho bila kulazimishwa ambapo amewataka waendelea kuboresha mashamba yao ili wapate korosho bora zitakazokubali kwenye soko la ndani na nje ya nchi.
“Nawashukuru wakulima kukubali kuuza korosho bila kulazimishwa kwani mmesikia kwenye mikoa ya wenzetu korosho zilibaki bila kununuliwa,sisi Ruvuma tulikuwa na kilo milioni 6.3 na zote zimeuzwa,tunamshukuru Mwenyezimungu kwa jambo hili”alisema Manjaule.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa TAMCU Marcelino Mrope amesema,katika mnada wa kwanza wa ufunguzi wa mauzo ya korosho ghafi katika Mkoa wa Ruvuma korosho zilizoingizwa kwenye mnada huo ni kilo milioni 6,354,190.
Aidha amesema,katika msimu 2024/2025 walifanya minada 9 na kuuza jumla ya kilo 31,608,038.0 zenye thamani ya Sh.93,014,553,825.00 sawa na ongezeko la asilimia 58.39 ukilinganisha na msimu 2023/2024 ambao walikusanya na kuuza kilo 26,062,323 zilizowaingizia wakulima Sh.45,451,569,135.50.
Amesema,katika msimu 2024/2025 mfumo uliotumika katika kuuza korosho ni wa stakabadhi ghalani na korosho zote ziliuzwa kwa utaratibu wa minada ya kimtandao unaosimamiwa na Soko la Bidhaa Tanzania(TMX) ambapo bei ya wastani ilikuwa Sh.1,747.41 kwa kilo moja.
Mkulima wa korosho wa Kijiji cha Nakapanya Hussen Kassim amesema,bei zilizotolewa kwenye mnada wa kwanza ni kidogo na amewaomba wanunuzi kuongeza kwenye minada mingine itakayofanyika.
Said Aidal amesema,korosho zinatumia gharama kubwa kwenye uzalishaji hivyo ni vyema wanunuzi waongeze fedha ili wakulima waweze kunufaika kutokana na zao hilo.
MWISHO.
Picha no 371 Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma(TAMCU LTD)Marcelino Mrope akitoa taarifa ya kuanza kwa minada ya korosho katika Mkoa wa Ruvuma.
Picha no374 Baadhi ya wakulima wa zao la Korosho Mkoani Ruvuma,wakifuatilia ufunguzi wa mnada wa korosho uliofanyika katika kijiji cha Nakapanya Wilayani Tunduru.
Picha no386 Katibu Tawala wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Milongo Sanga,akizungumza na wakulima wa korosho wakati wa ufunguzi wa mnada wa kwanza wa zao hilo uliofanyika katika kijiji cha Nakapanya wilayani humo.






