
Mhasibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) Samwel Oyee akitoa wasilisho kuhusu mambo muhimu katika kusimamia biashara wakati wa hafla ya ugawaji wa mikopo kwa walengwa wa Mfuko huo iliyofanyika tarehe 14 Novemba, 2025 katika ukumbi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake na Makundi Maalum iliyopo Mtumba Jijini Dodoma.
Baadhi ya wanufaika wa Mkopo wa Mfuko wa maendeleo ya wanawake (WDF) waliohudhuria hafla hafla ya utoaji mikopo na mafunzo kwa wanawake wajasiriamali iliyofanyika tarehe 14 Novemba, 2025 katika ukumbi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake na Makundi Maalum iliyopo Mtumba Jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felista Mdemu akigawa hundi ya Shilingi Milioni 337 kwa wanufaika wa Mkopo wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) tarehe 14 Novemba, 2025 katika ukumbi wa Wizara hiyo uliopo Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma. (Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini- WMJJWM)
Na. Jackline Minja WMJJWM- Dodoma.
Serikali amewataka wanufaika wa mikopo ya Mfumo wa Wanawake (WDF) kutumia mikopo wanayopata kukuza biashara zao ili kujikwamua kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu wakati akifungua hafla ya utoaji mikopo na mafunzo kwa wanawake wajasiriamali waliokidhi vigezo na kuidhinishwa Mikopo.
Mdemu amesema Serikali inatoa mikopo hiyo ikiwa ni utekelezaji Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2023 ambayo imelenga kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika nyanja zote za maendeleo na itaendelea kuweka mazingira wezeshi, Sera bora na programu bunifu za kuwaendeleza wanawake ili wachangie ipasavyo pato la Taifa na maendeleo ya nchi.
Mdemu amesema Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) ni tofauti na mifuko mingine kwa kuwa una sifa ya kipekee kwa kutoa mikopo yenye masharti na riba nafuu kwa walengwa ambao ni mwanamke binafsi na vikundi na hadi sasa jumla ya vikundi 4 vya wanawake wajasiriamali na wakopaji binafsi 25 wamepokea jumla ya Shilingi Milioni 337.
“Jambo hili halikuja kwa bahati mbaya bali ni dhamira ya dhati ya Serikali ya kuhakikisha wanawake ambao kutokana na vikwazo vya kimila na kitamaduni wamekuwa hawazifikii fursa za kiuchumi kwa ustawi na maendeleo yao na familia kwa ujumla. Hivyowito wangu kwenu mliopata mkopo leo hii, mkawe chachu ya kuutangaza mfuko na miradi yenu iwe kielelezo cha mfano na ushahidi katika jamii kuthibitisha tija ya mikopo inayotolewa na mfuko”. amesema Mdemu
Aidha amewataka wanawake waliopewa mikopo hiyo kufuata maelekezo ya mafunzo yaliyoandaliwa mahsusi ili kuimarisha uelewa kuhusu mkopo pamoja na kuhakikisha wanairejesha kwa wakati ili kusaidia mfuko kuendelea kutoa huduma kwa wanawake wengi nchini kote.
“Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wote mnaopokea mikopo leo hii kuzingatia maelekezo ya mafunzo yaliyoandaliwa mahsusi ili kuimarisha uelewa wenu kuhusu mkopo na mfuko unaowapatia mkopo, kutumia mkopo kulingana na malengo ya mradi kwa maana ya kuhakikisha fedha za mkopo zinatumika katika miradi uliowasilisha au kuombea, na si vinginevyo” amesisitiza Mdemu
Eleweni mkopo huu si msaada bali unapaswa kurejeshwa, hivyo ni muhimu kukuza mtaji, Mkopo una muda wa urejeshaji na mkopaji anapaswa kurejesha kwa wakati na kwa kufanya hivyo kutasaidia mfuko huu kuendelea kutoa huduma kwa wanawake wengi zaidi nchini kote”. ameongeza Mdemu.
Kwa upande wao wanufaika wa Mikopo hiyo wameishukuru Serikali kwa kuwaletea mikopo hiyo ambayo itawasaidia katika kukuza mitaji yao na kuongeza biashara zao ili kuendelea kuliongezea pato la Taifa.
“Tunaishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kutuona wanawake katika nyanja nyingi ikiwemo hii ya mikopo ambayo itakayotusaidia kukuza mitaji yetu, kuongeza biashara na kufanya kuwa na vipato vitakavyoongezeka katika kuliongezea pato taifa, lakini pia tunaishukuru Wizara hii kwa kuratibu zoezi hili hivyo niwaombe na wanawake wengine kuchangamkia fursa hii ili wanawake tupunguze utegemezi”.
wamesema wafanyabishara hao.






