Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema mkoa huo ni kitovu cha viwanda na ukanda wa miradi ya kimkakati, hivyo amewahimiza wawekezaji wa ndani na nje kuchangamkia fursa zilizopo.
Amesema Pwani inaendelea kuwa eneo la dira ya uwekezaji kutokana na upatikanaji wa miundombinu rafiki ikiwemo barabara, reli, bandari, umeme na ardhi iliyotengwa mahsusi kwa ajili ya viwanda na shughuli za uzalishaji.
Kunenge alitoa wito huo Novemba 25, 2025 wakati akimpokea Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Yordenis Despaigne Vera, aliyefika kutembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Ruvu kama sehemu ya kumbukizi ya kifo cha Rais wa zamani wa Cuba, marehemu Fidel Alejandro Castro, ambaye aliwahi kutembelea shule hiyo iliyojengwa kwa msaada wa Cuba.
Alisema mkoa una fursa pana za uwekezaji katika kujenga ujenzi wa viwanda vya chanjo na afya, sekta ya utalii, hoteli, umwagiliaji, kilimo, madini na afya, ambapo ardhi ya kutosha imetengwa kwa miradi hiyo.
“Mkishakuwa tayari, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mama. Amefanya kazi kubwa katika sekta ya mama na mtoto, na atafurahi mkiwekeza katika eneo hili kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto,” alieleza Kunenge.
Aidha, alibainisha kuwa ndani ya kipindi cha miaka minne, jumla ya viwanda 244 vimejengwa mkoani Pwani, sawa na wastani wa viwanda 61 kwa mwaka, hatua inayothibitisha kasi ya mkoa katika kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda.
Kwa upande wake, Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Yordenis Despaigne Vera, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushindi alioupata na kuaminiwa kuliongoza Taifa kwa miaka mitano ijayo.
Alikumbusha kuwa mnamo mwaka 1977, wakati wa uhai wa Fidel Castro, kiongozi huyo alitembelea Tanzania na kuchagua mkoa wa Pwani kutembelea Shule ya Kilimo Ruvu na Kituo cha JKT Ruvu, jambo lililoweka alama ya kipekee ya urafiki kati ya Tanzania na Cuba.
“Kwetu sisi mkoa huu una alama maalum, hapa ndiko zilipojengwa shule mbili Ruvu na Kibiti na kiwanda cha viuatilifu Kibaha ambacho kimekuwa nguzo katika mapambano dhidi ya malaria,” alisema Vera.
Aliongeza kuwa Cuba itaendelea kuuthamini na kuuendeleza ushirikiano ulioekwa na waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Fidel Castro.
Hata hivyo, Vera alieleza kuwa Cuba bado inapitia changamoto za kiuchumi kutokana na vikwazo vya kiuchumi vinavyoathiri sekta mbalimbali za kijamii nchini humo.
Ubalozi wa Cuba nchini unaendelea kuenzi kumbukizi ya Muasisi wa nchi hiyo, Hayati Fidel Alejandro Castro, aliyezaliwa Agosti 13, 1926 na kufariki Novemba 25, 2016 akiwa na umri wa miaka 90.






@1730665627.jpg)

@1730665594.jpg)



