Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuweka mikakati madhubuti na kutafuta suluhisho la kudumu dhidi ya changamoto ya upungufu wa maji katika Mto Ruvu hususani katika kipindi kirefu cha ukosefu wa mvua.
Amesema kwa kuwa changamoto hii ya upungufu wa maji katika vyanzo vya maji hususani Mto Ruvu huwa inatokea mara kwa mara, ni vyema Watendaji na Wataalamu kukaa na kuweka mikakati ya kudumu ya namna ya kutatua changamoto hii.
“Kutokana na hali hii, DAWASA mnakabiliwa na jukumu la kubuni miradi ya maji ambayo itawezesha kupatikana kwa huduma ya maji kwa kipindi chote cha upungufu wa majisafi, na ili kuweza kukidhi mahitaji ya maji kwa wananchi wa DaresSalaam,” amesema Mhe. Chalamila.
Mbali na hapo, ameitaka DAWASA kuwekeza nguvu katika kufufua visima vilivyopo vya maji ili viweze kutoa huduma na kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu upungufu wa huduma.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DAWASA Mhandisi Romanus Mwangingo amesema kuwa Mamlaka imepokea maelekezo yote na kazi inaendelea ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ikiwemo kutoa maji kwa mgao sawia katika maeneo yote ya Jiji.
Ameongeza kuwa jitihada mbalimbali zinaendelea kutekelezwa ikiwemo, kufufua visima vilivyopo vya maji kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa maji na kupunguza makali ya uhaba wa huduma kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi wa Bonde la Wami Ruvu Mhandisi Elibariki Mmasi amesema kuwa changamoto hii iliyotokea ni kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri maeneo mengi ya kihuduma na kusababisha vyanzo vya maji kupungua.
“Hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwemo kusitisha utoaji wa vibali kwa Watumiaji wa skimu za umwagiliaji katika kipindi hiki cha kiangazi kwa lengo la kuimarisha wingi wa maji,” amesema Mhandisi Mmasi.








