NA DENIS MLOWE, IRINGA
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa leo imeadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Mahakama Kuu Iringa, ikiongozwa na kauli mbiu isemayo “Safari ya Miaka 20 ya Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Iringa tulipotoka, tulipo na tunapokwenda.”
Mahakama hiyo ilianzishwa rasmi mwaka 2005, ambapo majengo yake yalizinduliwa na Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa, na imekuwa ikihudumia mikoa ya Iringa na Njombe.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi wa Mahakama, watumishi wa Mahakama, viongozi wa Serikali, viongozi wa kisiasa, viongozi wa kimila pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Jaji Kiongozi wa Tanzania, Mheshimiwa Mustapha Siyani, aliyewakilishwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mheshimiwa Imani Aboud.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Kheri James, ametoa pongezi kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kwa kuendeleza mahusiano mazuri kati ya Mahakama na Serikali, yakiwemo mahusiano na Mawakili wa Serikali na Mawakili wa kujitegemea. Amesisitiza kuwa amani ni tunda la haki na maendeleo ni zao la haki, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuilinda na kuiendeleza haki kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
Mheshimiwa Kheri James ameongeza kuwa ili haki itendeke kwa wakati, ni muhimu kwa taasisi zote zenye mamlaka ya kushughulikia haki, ikiwemo Jeshi la Polisi, Magereza na TAKUKURU, kutoa ushirikiano wa karibu kwa Mahakama, hususan katika utoaji wa ushahidi kwa wakati. Aidha, amewahimiza wananchi kuendelea kulinda haki na amani ya taifa.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mheshimiwa Dunstan B. Ndunguru, amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Mahakama hiyo mwaka 2005, maboresho makubwa yamefanyika ikiwemo kuimarika kwa utoaji wa haki, uboreshaji wa majengo, matumizi ya TEHAMA na kuongezeka kwa kasi ya usikilizaji wa mashauri.
Ameeleza kuwa majengo ya Mahakama hayo awali hayakusanifiwa mahsusi kwa ajili ya Mahakama, lakini baada ya kufanyiwa usanifu na maboresho, sasa yamekidhi viwango vya Mahakama Kuu na kuwezesha shughuli zote kufanyika kikamilifu.
Jaji Ndunguru ameongeza kuwa katika kuadhimisha miaka 20, Mahakama imejipanga kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati, kuimarisha weledi kwa watumishi, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ili kuongeza uelewa wa haki zao. Amesisitiza kuwa Mahakama itaendelea kudumisha mafanikio yaliyopatikana na kuendeleza utoaji wa haki sawa kwa wote.
Akihitimisha, mgeni rasmi ametoa pongezi kwa uongozi na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, akisisitiza kuwa Mahakama si jengo bali ni mfumo unaojengwa na wananchi, wadau na watoa haki. Ameeleza kuwa hakuna sababu ya kuchelewesha mashauri bila sababu za msingi, na kila mtumishi anapaswa kuwa sehemu ya kujenga heshima ya muhimili wa Mahakama.
Aidha, amewahimiza Majaji na Mahakimu kufanya kazi kwa kujituma, umahiri na weledi kwa kuzingatia Sheria na Katiba, na kutoa haki kwa kusimamia viapo vyao vya kazi, akisisitiza kuwa taswira ya haki inalenga utu, usawa na weledi katika utendaji wa haki.









