*Lengo ni Kulinda maslahi ya Taifa na kuweka Mazingira Bora kwa Wawekezaji
*Ameeleza kuwa EWURA ni Taasisi Muhimu kwa usalama wa Nchi.
*Asisitiza uwepo wa Akiba ya Mafuta kwa ajili ya dharura.
Waziri wa Nishati, Mhe. Deugratius Ndejembi, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuhakikisha inatenda haki kwa wawekezaji katika sekta ya mafuta bila upendeleo wowote, na kusisitiza kuwa maamuzi yote yafanywe kwa kuzingatia sheria, taratibu na haki, na siyo kwa kuangalia majina au watu binafsi, ili kulinda mazingira bora ya uwekezaji nchini.
Mhe. Ndejembi ametoa maagizo hayo Desemba 19, 2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza na Viongozi na Watendaji wa EWURA lengo likiwa ni kujitambulisha na kuona shughuli wanazozifanya.
“Kuna baadhi ya watendaji wa EWURA hutumia madaraka vibaya kwa kuwaonea wawekezaji, wa vituo vya mafuta kwa kuvifunga na baadhi ya vituo vingine vyenye changamoto kama hiyo kuachwa, hivyo nasisitiza hali hii isiwepo kwani nikibaini uonevu huo hatua za kinidhamu zitachukuliwa hivyo tuzingatie haki na usawa katika utekelezaji wa majukumu yetu kwa maslahi ya Taifa letu.
EWURA ni Taasisi Muhimu kwa usalama wa Nchi yetu hivyo tuhakikishe tunaweka maslahi ya Taifa mbele ili kuboresha ustawi wa Watanzania sambamba na kukuza uchumi wa nchi yetu huku tukihakikisha tunaweka akiba ya mafuta kwa ajili ya kukabiliana na dharura”. Amesisitiza Mhe.Ndejembi.
Aidha Mhe. Ndejembi amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji na uadilifu kwa watumishi wa EWURA na kwamba hatomvumilia mtumishi yeyote ambaye atakwenda kinyume na sheria, taratibu na kanuni za kiutumishi .
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mhandisi Innocent Luoga ameipongeza menejimenti ya EWURA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha sekta ya mafuta inaendelea kukua huku akieleza kuwa Wizara ya Nishati inaendelea kushirikiana na Taasiai zake kuhakikisha maelekezo na vipaumbele vya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan vinatekelezwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt. James Andilile ameeleza kuwa EWURA imeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya gesi asilia kwenye magari (LPG) pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta maeneo ya Vijijini.







