

Jeshi la Polisi Tanzania linapenda kuwajulisha wananchi kuwa, leo ni takribani siku ya kumi tangu kutolewa kwa taarifa ya hali ya usalama nchini tarehe 12/12/2025, na kwa kipindi chote hicho hali ya usalama nchini imeendelea kuwa shwari.
Hali hiyo imedumishwa licha ya kujitokeza kwa matukio machache ya kiusalama ambayo yalishughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa Sheria za nchi pamoja na mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa.
Ushwari huu unatokana na uelewa wa Watanzania kuhusu umuhimu wa kulinda na kuimarisha amani, utulivu na usalama, ambavyo ni misingi muhimu inayowezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli halali za kiuchumi na kijamii.
Tunapoelekea kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka mpya, zitakazotanguliwa na sherehe za Krismas, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama linaendelea kuimarisha ulinzi wakati wote wa sikukuu na hata baada ya sikukuu hizo.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote na wageni waliopo nchini kuendelea kuthamini na kulinda amani na usalama, pamoja na kuyakataa vitendo au mienendo yenye lengo la kuvuruga amani katika kipindi hiki cha sikukuu na kuendelea mbele.
Aidha, Jeshi la Polisi linawakumbusha wasafiri wote kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani ili kuepuka ajali, tukizingatia kaulimbiu ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani isemayo:
“Endesha Salama, Familia Inakusubiri.”
Imetolewa na:
Msemaji wa Jeshi la Polisi
Makao Makuu ya Polisi
Dodoma, Tanzania

The post Polisi Waendelea Kuimarisha Ulinzi Nchini Kuelekea Sikukuu – Video appeared first on Global Publishers.







