*- Wasema machafuko, uchochezi na uharibifu wa miundombinu vimefeli; wachagua amani kulinda ajira, biashara na Taifa
Dar es Salaam.
Wajasiriamali wa kada mbalimbali kutoka wilaya zote tano za Mkoa wa Dar es Salaam wametoa msimamo mkali wakikemea vurugu, machafuko na uchochezi, wakisisitiza kuwa vitendo hivyo havina uwezo wa kutatua changamoto za wananchi, bali vinachoma ajira, vinaharibu biashara na kuumiza mustakabali wa Taifa.
Wakizungumza kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa leo, wajasiriamali hao walisema kuwa ingawa wao kama wadau wengine wana changamoto, madai, matamanio na mahitaji halali, uzoefu wa vurugu za Oktoba 29 umeonesha wazi kuwa njia ya vurugu si suluhu ya matatizo ya wananchi.
“Tunayo changamoto zetu kama wajasiriamali, tunayo madai na mahitaji halali, lakini tumejifunza kwa gharama kubwa kwamba vurugu, uchochezi na uvunjifu wa amani haviwezi kamwe kuleta suluhu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
*WALAANI MADHARA YA OKTOBA 29
Katika msimamo wao, wajasiriamali walieleza masikitiko makubwa na maumivu ya dhati kwa madhara yaliyowakumba wakazi wa Dar es Salaam kufuatia machafuko hayo, yakiwemo:
• uharibifu wa miundombinu ya mabasi ya mwendokasi, uliosababisha watumishi kukosa ajira au kipato na wananchi kukosa huduma muhimu ya usafiri;
• kuchomwa kwa taasisi na maeneo ya biashara, hali iliyowaathiri wajasiriamali wenzao na wafanyakazi waliokuwa wameajiriwa katika maeneo hayo;
• pamoja na vifo, majeruhi na madhara mengine ya kibinadamu, yaliyoacha majonzi kwa familia na jamii kwa ujumla.
Wajasiriamali hao wamesema wazi kuwa hakuna hoja, madai wala ajenda yoyote inayoweza kuhalalisha uharibifu wa miundombinu ya umma, kuchomwa kwa mali za watu au kupotea kwa maisha ya wananchi, wakisisitiza kuwa hali hiyo si ya kujivunia kama Taifa.
*WANAHARAKATI NJE NA WANASIASA WALAUMIWA
Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa vurugu na uchochezi huo umekuwa ukihamasishwa na wanaharakati waliojificha nje ya nchi, pamoja na baadhi ya wanasiasa wa vyama fulani hapa nchini, wanaotumia hasira za wananchi kama mtaji wa kisiasa bila kujali athari zake kwa wananchi wa kawaida.
“Wanaohamasisha vurugu hawabebi gharama zake. Gharama zinabebwa na mjasiriamali, mfanyakazi na familia masikini,” ilieleza taarifa hiyo.
*WAPINGA MATUMIZI YA GEN-Z KATIKA VURUGU
Wajasiriamali hao walikemea pia propaganda zinazotumia kizazi cha Gen-Z kuhalalisha vurugu, fujo na ukosefu wa maadili, wakisisitiza kuwa vijana hao wanapaswa kuonekana kama nguvu kazi yenye tija na mustakabali wa Taifa, si chombo cha uharibifu.
*“NI MIMI” – MSIMAMO WA MWISHO*
Katika hitimisho yao, wajasiriamali walisisitiza falsafa ya “NI MIMI”, wakisema kila raia ana wajibu binafsi wa kulinda amani.
*“Tunasema wazi kuwa ‘MIMI’ ndiye NCHI, ‘MIMI’ ndiye Serikali, na ‘MIMI’ ndiye mwenye wajibu wa kulinda amani, uchumi na ustawi wa Taifa,” ilisema taarifa hiyo.
Waliwahamasisha wajasiriamali wengine ndani ya Dar es Salaam na nchini kote kuwa daraja la kutatua changamoto kwa njia sahihi, kupitia mazungumzo, mifumo halali ya kisheria na uwajibikaji wa raia, si kwa vurugu, uchochezi wala uharibifu wa miundombinu.
Kwa kauli moja, wajasiriamali hao walisema:
“Tunakataa vurugu. Tunakataa uchochezi. Tunakataa uharibifu. Tunachagua amani kama njia pekee ya kulinda ajira, biashara na mustakabali wa Taifa.”









