Na Happy Lazaro,Arusha .
Mkuu wa wilaya ya Arusha Joseph Mkude amewataka madiwani wa halmashauri ya jiji la Arusha kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya afya kwa wote(NHIF) ili kuwa na uhakika wa matibabu.
Ameyasema hayo leo wakati akizundua mpango wa bima ya afya kwa wote iliyofanyika katika ofisi za mkuu wa wilaya ya Arusha .
Mkude amesema kuwa, ni vyema madiwani wakatoa elimu kwa wananchi wao katika kata kwa kuwa serikali imeweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wananchi wote kujiunga na mfuko huo .
“Ninyi madiwani ndio mnaoishi na wananchi katika kata zenu hivyo niwaombe kwenda kutoa elimu kwa wananchi wote kwa kuwa azma ya serikali ni kila mwananchi awe na uhakika wa matibabu kwa gharama nafuu bila kumwacha mwananchi yoyote asiwepo wa kukwamisha .”amesisitiza Mkude.
Aidha amewatoa hofu wananchi kwa kusema kuwa mfuko wa bima ya afya kwa wote umeboreshwa kwa kuwa changamoto zote za awali zilizokuwa zinakwamisha mwananchi kupata huduma zozote zimeshughulikiwa hivyo wananchi wachangamkie fursa hiyo ili kuwa na uhakika wa matibabu kwa gharama ambayo ni nafuu sana .
“Changamoto zote za kukosa dawa , ucheleweshaji wa matibabu na baadhi ya vipimo serikali yenu imeziangalia na kuzifanyia kazi ukiwa na bima hii utapata matibabu popote na kwa wakati na bila usumbufu wowote hivyo tuiunge mkono serikali ya awamu ya sita ya Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuchangamkia fursa hii na kuhakikisha hakuna anayeachwa kwa kuwa suala la afya ni swala la wote “amesema Mkude.
Kwa upande wake Afisa uanachama kutoka NHIF Miraji .Kisile amesema kuwa, Swala la bima lisiwe swala la hiari bali liwe swala.la utekelezaji wa kisheria ambapo katika utekelezaji wa sheria hiyo serikali imeandaa mpango mahususi kabisa wananchi kuwa na mfumo wa uchangiaji katika bima ya afya kwa gharama nafuu ili waweze kupata huduma kadri ya mahitaji waliyonayo.
“Kupitia sheria ya mfuko wa bima ya afya imeainisha kuwa makundi mbalimbali ambapo kundi mojawapo ni kundi la watumishi wa umma kwa lazima sasa wote watatakiwa kuwa wanachama wanaochangia katika mifuko mbalimbali ya bima ya afya hata yale makundi ambayo serikali inashare asilimia.chache waweze kuwa katika utaratibu wa bima ya afya na kuweza kuchangia kuharakisha ukuaji wa sekta ya afya .”amesema Kisile .
Amesema kuwa sheria inaenda kulazimisha wafanyakazi wa sekta binafsi yakiwemo makampuni mbalimbali ya watu binafsi pamoja na taasisi na mashirika ya kijamii ambayo siyo ya kiserikali lazima wafanyakazi wake wawe wanachama katika mifuko ya bima ya afya .
“Lakini pia kuna makundi mengine yameweza kutambuliwa ambayo ni makundi muhimu kabisa likiwemo kundi la wajasiriamali mbalimbali,baba lishe ,mama lishe vijana wa boda boda wamachinga na wajasiriamali wengine wote wanapata fursa ya kuweza kuunganishwa katika huo utaratibu katika mifuko ya bima ya afya na wao wamewekewa utaratibu namna ambavyo watachangia .”amesema Kisile.
Aidha amefafanua kuwa,kuna kundi la.wazee wasiojiweza pamoja na kaya maskini ambapo serikali.imeweka utambuzi wa kaya maskini ambapo kaya hizo zitaendelea kutambuliwa na serikali.







