NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amezitaka taasisi zote za serikali mkoani humo kuongeza umakini katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kwamba hakuna manufaa kujenga majengo bila huduma muhimu kama maji, umeme na barabara.
Akizungumza kwenye kikao kazi cha kutembelea miradi ya maendeleo katika ziara ya siku mbili aliyoanza jana katika wilaya ya Kilolo ,Mkuu wa Mkoa alisema kuwa miradi mingi imekuwa ikikamilishwa kimajengo lakini inashindwa kufanya kazi kwa sababu miundombinu tegemezi haikuhusishwa tangu mwanzo.
“Huwezi kusema umeleta mradi wa milioni 65 halafu ukashindwa kuhakikisha maji ya milioni 20 yanapatikana. Hilo linaidhalilisha serikali,” alisema.
Alizitaka taasisi kama TARURA, TANESCO, Mamlaka za Maji na Sekta ya Afya kujipanga kwa pamoja na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wakati ujenzi wa miradi inayoendelea.
“Kabla ya mradi kuanza, jiulize – unahitaji maji? Barabara? Umeme? Mtandao? Hayo yote yanapaswa kuandaliwa sambamba. Hatutaki ukamilifu wa nusu nusu,” alisisitiza Kheri James
Aonya hatari za kukosekana kwa huduma
Akitoa mfano, alisema kuwa kujenga shule bila maji ni kuhatarisha afya za watoto na walimu.
“Tukijenga shule nzuri bila maji, tutatengeneza mazingira ya magonjwa ya mlipuko. Tutakuwa tunawaumiza watoto badala ya kuwalinda,” alisema.
Atoa maelekezo kwa viongozi wa vijiji na kata ambapo Mkuu wa Mkoa amewataka wenyekiti wa vijiji na vitongoji kuhakikisha maeneo ya huduma kama shule, zahanati na ofisi za kijiji yanapangwa mapema na kupimwa, kisha kulindwa dhidi ya uvamizi.
“Tusipange maeneo leo, kesho tutapata pesa za miradi lakini maeneo hakuna. Hakikisha eneo la huduma haligeuki kuwa makazi ndani ya siku mbili,” alisema.
Ametoa pia wito kwa viongozi kuhamasisha wazazi kuwaandaa watoto kurudi shule, akisisitiza hakuna mtoto anayepaswa kubaki nyumbani.
Asisitiza utunzaji wa mazingira katika miradi ya afya
Katika ziara yake kituo cha Afya cha Ilula, Rc Kheri James ametoa rai kupanda miti ya kivuli, matunda, dawa na miti ya matumizi kwenye majengo yote ya serikali.
Awapongeza watumishi wa afya, awaahidi ajira za serikali
Mkuu wa Mkoa aliwapongeza watumishi wa afya kwa huduma nzuri na kuahidi kuwa vijana wanaojitolea hawatasahaulika.
“Ni suala la muda tu. Serikali itaendelea kuwaajiri kwa awamu. Tunatambua kazi kubwa wanayofanya,” alisema.
RC Kheri James alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kusimamia ipasavyo miradi ya wananchi na kuweka mbele maslahi ya umma.
Mkuu wa mkoa yuko katika ziara ya kutembelea wilaya zote za mkoa wa Iringa katika kukagua miradi ya maendeleo ambapo kesho atakuwa wilaya ya Iringa.






