Na. Ofisi za Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Ofisi za Halmashauri ya Jiji la Dodoma zitakuwa wazi siku ya Jumamosi tarehe 10 Januari, 2026 kuanzia saa 2:30 hadi saa 9:30 alasiri kwa lengo la kuwahakikishia huduma bora hasa upatikanaji wa ‘control number’ za malipo ya viwanja ndani ya muda wa notisi ya halmashauri ya siku 21.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dennis Gondwe alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu maelekezo ya Mkurugenzi wa Jiji hilo juu ya ofisi hizo kufunguliwa siku ya Jumamosi, tarehe 10 Januari, 2026.
“Ndugu waandishi wa habari, napenda kuwatangazia kuwa katika kufanikisha utekelezaji wa Notisi ya siku 21 ya kulipa madeni ya viwanja kwa wananchi waliochukua viwanja eneo la Mtumba Zone II, III na Kikombo kuanzia tarehe 30 Desemba, 2025 inayokamilika tarehe 19 Januari, 2026. Hivyo, mkurugenzi ameagiza ofisi za halmashauri iliyokuwa manispaa ya zamani duka la kuuza viwanja ziwe wazi kuanzia saa 2:30 asubuhi hadi saa 9:30 alasiri” alisema Gondwe.
Akiongelea umuhimu wa agizo hilo, alisema kuwa linalenga kuwarahisishia wananchi huduma bora na za haraka katika kulipia madeni ya viwanja hivyo. “Halmashauri inaamini kuwa wapo baadhi ya wadaiwa wa viwanja ambao kwa asili ya kazi zao hawakupata nafasi katikati ya wiki kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa ya kufika duka la kuuzia viwanja kupata ‘control number’. Hivyo, siku ya Jumamosi tarehe 10 Januari, 2026 itakuwa ni siku muhimu sana kwa wananchi kupata huduma. Aidha, ofisi hizo zitakuwa wazi pia Jumamosi ya tarehe 17 Januari, 2026” alisema.
Akijibu swali kuhusu mpango wa halmashauri kuongeza muda baada ya kukamilika kwa Notisi ya siku 21, alisema kuwa wadaiwa wa viwanja wakamilishe malipo hayo sasa. “Leo ni siku ya 11 ya utekelezaji wa wa Notisi ya halmashauri, hivyo, kwa sasa halmashauri haifikirii kuongeza muda kwa wadaiwa wa viwanja. Orodha ya wateja wapya wanaosubiri viwanja hivyo ni kubwa” alisema Gondwe.
Kwa upande wake Adam Juma mteja aliyefika kupata huduma ya kulipia kiwanja Halmashauri ya Jiji la Dodoma alipongeza kasi ya huduma inayotolewa. “Nimefurahishwa sana na huduma hii, nimekuja hapa kama dakika kumi tu, huu utaratibu ni mzuri sana kwasababu unatusaida kukamilisha uhakiki wa viwanja vyetu na malipo kwa ujumla. Nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Halmahauri ya Jiji la Dodoma kwa ufatiliaji na udhibiti huu wa ardhi zetu” alisema Adam






