Na Sabiha Kamis, Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Ascending Africa kupitia mradi wa Jahazi wanatarajia kufanya mkutano wa Kikanda wa Kukabiliana na Uvuvi Haramu na Kukuza Uchumi wa Buluu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ya Zanzibar Kapten Hamad Bakar Hamad imesema kuwa lengo la mkutano huo ni kuimarisha uongozi wa Afrika katika usimamizi wa bahari, kuendeleza uchumi wa buluu unaozingatia uendelevu, na kuimarisha hatua za pamoja za kukabiliana na Uvuvi Haramu katika ukanda wa Bahari ya Kusini-Magharibi mwa Bahari ya Hindi.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mkutano huo wa siku tatu utafanyika kuanzia tarehe 26 hadi 28 Januari 2026, na utakutanisha serikali, taasisi za kikanda, wadau, wataalamu wa bahari, na washirika wa maendeleo kutoka nchi za Mauritius, Kenya, Tanzania na Zanzibar.
Aidha taarifa imefahamisha kuwa ushirikiano huo unaakisi vipaumbele vya pamoja vya nchi za Kusini-Magharibi mwa Bahari ya Hindi ambazo zinakabiliwa na changamoto katika matumizi endelevu ya rasilimali za baharini, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabianchi, na ustawi wa jamii za pwani.
Imesema kuwa kupitia Mkutano huo wa (Sauti za Buluu) 2026, nchi washiriki zinalenga kujenga mwitikio wa kikanda unaojikita katika ushirikiano wa dhati, uwazi wa mifumo ya usimamizi wa bahari, na utekelezaji wa sera, sheria na mikakati ya bahari.
Hata hivyo taarifa hiyo imesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeeleza kuwa changamoto zinazokabili bahari katika ukanda wa SWIO haziwezi kutatuliwa na taifa moja pekee, bali zinahitaji mshikamano wa kikanda hivyo kupitia uongozi wake katika kuandaa Mkutano Zanzibar inalenga kuimarisha diplomasia ya bahari, kukuza ushirikiano wa kikanda, na kuweka msingi wa hatua za pamoja dhidi ya uvuvi haramu.
“Zanzibar imejidhatiti kushirikiana kwa karibu na nchi jirani katika ukanda wa Kusini-Magharibi mwa Bahari ya Hindi kulinda bahari yetu ya pamoja, mkutano wa Blue Voices 2026 unatupa jukwaa muhimu la kuimarisha mshikamano wa kikanda, kuendeleza suluhu za vitendo, na kuongeza ufanisi wa mapambano dhidi ya uvuvi haramu. Ushirikiano wa kikanda ndio msingi wa kulinda rasilimali zetu za baharini na kuhakikisha ustawi wa jamii zinazotegemea bahari.” Imeeleza Katibu Mkuu.
Nae Msemaji wa Mradi wa Jahazi Michael Mallya amesema kuwa mkutano wa Blue Voices 2026 ni hatua muhimu katika kuinua uongozi wa Afrika katika masuala ya usimamizi wa bahari.
“Mkutano huu unaashiria mwanzo wa sura mpya katika usimamizi wa bahari Afrika Mashariki na Ukanda wa Kusini-Magharibi mwa Bahari ya Hindi kwa Ujumla kwani Uvuvi haramu hustawi pale mifumo inapokuwa imegawanyika na ushirikiano ukiwa dhaifu hivyo kupitia mshikamano wa kikanda, nchi za Mauritius, Kenya, Tanzania na Zanzibar zinajitokeza kwa sauti moja kuchukua umiliki wa bahari zetu na mustakabali wa kizazi kijacho,” ameeleza Mallya.
Amesema wadau wa sekta ya uvuvi, uhifadhi wa mazingira, uchumi wa buluu, na usalama wa chakula wanautazama mkutano wa Blue Voices 2026 kama fursa muhimu ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mikataba, ahadi na mifumo ya kikanda iliyopo.
Amesema Mkutano huo unalenga kuunda mfumo wa muda mrefu wa usimamizi wa bahari kwa ushirikiano, unaotoa manufaa endelevu ya kimazingira, kijamii, na kiuchumi kwa jamii za pwani katika ukanda wa huo.
Mkutano huo utaendeshwa chini ya kauli mbiu ya “Bahari Moja, Sauti Moja (One Ocean, One Voice)”, ikisisitiza ukweli kwamba bahari ya ukanda huo ni rasilimali ya pamoja inayohitaji maamuzi ya pamoja na hatua shirikishi.
Kaulimbiu hiyo pia inaakisi dira ya muda mrefu ya Serikali ya Zanzibar ya kuitumia bahari kama nguzo kuu ya maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na kimazingira.





