NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Iringa Mjini, Mhe. Fadhili Ngajilo, ameagiza ukarabati wa haraka wa miundombinu katika soko la Olofea (Lavela) baada ya kufanya ziara ya kukagua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa eneo hilo.
Akiwahutubia wafanyabiashara, Mhe. Ngajilo alisema amefika akiwa na timu ya wataalamu wa Halmashauri ili kujiridhisha na kero zilizowasilishwa kwake mara kadhaa, zikiwemo vumbi jingi, miundombinu hafifu ya majiko, mabati yanayovuja maji, na changamoto za maji na umeme.
Mbunge huyo alisema moja ya kilio kikubwa ni mazingira duni ya kufanya biashara hasa msongamano wa vumbi wakati wa kiangazi na tope wakati wa masika.
“Natamani hapa ipigwe floor ya saruji. Wafanyabiashara wetu mnafanya kazi kwenye mazingira magumu sana,” alisema.
Aliongeza kuwa ndani ya wiki mbili, ofisi yake kwa kushirikiana na Manispaa itaweka mpango wa kuanza kazi hiyo ili kuboresha usafi na mazingira rafiki kwa biashara na hivyo Majiko na eneo la kupikia chakula kukarabatiwa
Mhe. Ngajilo alieleza kusikitishwa na hali ya eneo la majiko, akisema halina viwango vinavyostahili kwa sehemu inayohudumia chakula.
Aliahidi kukagua na kuweka mipango ya kuboresha miundombinu ya upishi ili kuhakikisha usalama, usafi na heshima kwa wafanyabiashara, wakiwemo kinamama wanaojishughulisha na uandaaji wa vyakula.
Akizungumzia huduma za maji na umeme, Mbunge Ngajilo alisema changamoto nyingi ni za kiutawala na usimamizi.
“Umeme mnauzwa mwingi lakini matumizi ni madogo. Haya ni matatizo ya management,” alisema.
Aliagiza utaratibu wa haraka kuwekwa ili kuhakikisha maji yanapatikana kwa wakati na gharama za huduma hizo zinakuwa zinazowiana na matumizi halisi kwani Lavela: Soko muhimu kwa uchumi wa Iringa
Mbunge huyo alisema zaidi ya asilimia 30 ya wakazi wa Iringa ni wafanyabiashara, hivyo masoko na minada ni uti wa mgongo wa uchumi wa mji.
Alisema soko la olofea linahudumia mamia ya watu kila siku na ndilo chanzo muhimu cha kipato kwa familia nyingi.
“Hapa kwa wastani zaidi ya watu 500 huingia kila siku kufanya shughuli zao. Hili ni eneo lenye umuhimu mkubwa,” alisema.
Amesema fedha za mfuko wa jimbo zitatumika kukamilisha maeneo ambayo hayajakamilika ili soko hilo liwe salama, la kisasa na rafiki kwa wafanyabiashara na wateja.
Akizungumzia kuhusu afya kwa Wote, Ngajilo awahamasisha wananchi kujiunga
na Bima ya Afya kwa Wote ambayo imeanza kutekelezwa chini ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Alieleza kuwa gharama ya 150,000 kwa familia ya watu sita inalenga kutoa unafuu mkubwa kwa kaya nyingi nchini.
Na kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Soko hilo, Abuja Peter, soko la Mitumba la HallFear lililopo katika Manispaa ya Iringa, kata ya Mshindo ametoa ufafanuzi kuhusu umuhimu wa soko hilo kwa wananchi wa Iringa na maeneo jirani.
Alisema kuwa Soko la hilo ni miongoni mwa masoko yaliyojengwa na Serikali kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa Peter, soko hili limekuwa msaada mkubwa kwa makundi mbalimbali, ikiwemo watu wenye uhitaji kutoka Mafinga, Wilaya ya Kilolo, Mtera na hata maeneo ya jirani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambao kwa njia tofauti wamenufaika na uwepo wa shughuli za kibiashara sokoni.
Aidha, soko hilo limekuwa tegemeo kubwa kwa akina mama wengi wa Iringa ambao familia zao zina kipato cha chini. Kwa wastani, soko hili linahudumia wafanyabiashara rasmi wapatao 500 kwa siku wengi wao wakiwa wauzaji wa nguo za mitumba.
Alisema kuwa kutokana na wingi wa wateja, soko hupokea hadi watu 600 kwa wakati mmoja, hivyo kuwalazimu kuingia kwa awamu tatu: asubuhi, mchana na jioni.
Katika upande wa uchumi, Soko la Vela limekuwa kichocheo muhimu kwa Manispaa ya Iringa na mkoa kwa ujumla. Wafanyabiashara hulipa ushuru, na shughuli sokoni huongeza mzunguko wa fedha kwa sekta nyingine kama boda boda, bajaji na wauzaji wa bidhaa mbalimbali wanaopata wateja kutoka sokoni.
Peter ameongeza kuwa soko hilo limekuwa sehemu ya ajira kwa vijana na watu wengi waliohitimu vyuo vikuu, lakini ambao hawakupata ajira rasmi.
“Ukija hapa, unachukua koti lako au shati lako, unalionyesha, mtu analinunua na anaendelea na safari. Mitumba yetu ni bora, mingi ni mipya kabisa za viwandani,” alisema.
Makamu Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wananchi wa Iringa na maeneo mengine kufika katika Soko la hil ili kunufaika na bidhaa nafuu na huduma zinazopatikana.
Soko liko wazi kwa wafanyabiashara kutoka maeneo yote bila masharti magumu, na linafikika kwa urahisi.






