KAMBI Maalumu ya Kibingwa ya Upasuaji wa Mdomo Sungura na Mdomo Wazi imezinduliwa rasmi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, ikihusisha madaktari bingwa kutoka ndani na nje ya nchi.Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mh. Kheri James, ambaye ametembelea maeneo ya utoaji huduma na kujionea maandalizi yaliyofanyika.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mh. Kheri James amesema Serikali ya Mkoa imejiandaa kikamilifu kuhakikisha kambi hiyo inaenda vizuri kuanzia mwanzo hadi mwisho, ili wagonjwa wapate matibabu bora na kuondoka wakiwa na tabasamu jipya.
Amewataka wananchi kuchangamkia fursa za kimatibabu pindi zinapotangazwa, akisisitiza kuwa kambi hii inahudumia watu wazima na watoto.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amelishukuru Shirika la Operation Smile kwa kuratibu kwa ukamilifu zoezi la kuwapata wagonjwa, kuwapatia malazi, matibabu na huduma nyingine muhimu.
Amesema ushirikiano mzuri kati ya Serikali ya Mkoa na shirika hilo umewezesha ujio wa madaktari kutoka nchi mbalimbali kuhudumia wananchi kwa kushirikiana na madaktari na wataalamu wa afya wa ndani.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dkt. Alfred Mwakalebela, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hii adhimu ya kupata huduma za kibingwa. Amesema hospitali kama mwenyeji wa kambi hiyo imehakikisha mazingira ni rafiki, vifaa tiba vinapatikana, na watumishi wake wanashiriki kikamilifu katika kutoa huduma hizo.
Dkt. Mwakalebela ameongeza kuwa wagonjwa wanaohudumiwa wanatoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania, jambo linalodhihirisha umuhimu wa kambi hiyo kwa taifa.
Kambi hiyo maalumu imeanza tarehe 07 Februari 2026 na inatarajiwa kukamilika tarehe 15 Februari 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.





