■Aipongeza BMH kupanua Wigo wa Huduma za Tiba Utalii kwa Wananchi wa nchi ya Malawi.
Na Jeremia Mwakyoma-BMH
DODOMA – MACHI 6, 2026
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio katika siku 100 za uongozi wake madarakani ambapo pamoja na maeneo mengine amesema katika kipindi hicho kumeakuwa na ongezeko la utoaji wa huduma za Kijamii kwa Wananchi zikiwemo za Afya na ongezeko la Utatuzi wa kero na changamoto za Wananchi.
Mhe. Senyamule pia ameipongeza Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) katika kipindi hiki cha siku 100 za Mhe Rais kwa kufanikiwa kupanua wigo wa utoaji wa huduma za Afya nchini na pia kwa kupanua huduma za Tiba Utalii kwa kufanikiwa kuanza kutoa huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi kwa Wananchi wa Malawi.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo wakati akifungua maonesho ya Taasisi za Umma zipatazo 35 katika Mkoa wa Dodoma zikiangazia mafanikio ya siku 100 za Mhe. Rais Samia Madarakani; maonesho ambayo yametoa fursa kwa Wananchi kutatuliwa kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili kupitia Clinic Maalumu za kutatua kero zinazoendeshwa na Taasisi mbalimbali za Umma kwenye viwanja vya Nyerere Square.
Hatua ya BMH kuanza kuwahudumia tiba utalii wananchi wa Malawi inafuatia ziazara ya viongozi wa BMH walipotembelea nchini Malawi na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Wizara ya Afya ya Malawi na baadae viongozi hao walitembelea BMH kujionea hali ya utoaji huduma za afya na sasa Wananchi wa Malawi wameanza kupata matibabu BMH.
Maonesho hayo yataendelea kufanyika katika Viwanja vya Nyerere Square hadi siku ya Ijumaa Machi 6, 2026 yatakapohitimishwa na BMH itaendelea kutoa huduma za Afya katika Viwanja hivyo ikiwemo matibabu ya moyo, Figo na Magonjwa ya Damu.




