Mgeni rasmi wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Bakhresa Group of Company Mwanafumo Mohamed akikata keki na Meneja wa Rasilimali watu Hospitali ya Dar Group Abdulrahman Muya na Mwenyekiti wa Chama cha wanawake Dar Group Agnes Mkama wakati wa hafla fupi ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani iliyofanywa na wanawake wa Hospitali hiyo jana jijini Dar es Salaam
Meneja wa Rasilimali watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Abdulrahman Muya akikabidhi zawadi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Bakhresa Group of Company Mwanafumo Mohamed wakati wa hafla ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani iliyofanywa na wanawake wa Hospitali hiyo jana jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
07/03/2026 Wanawake zaidi ya 200 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya saratani ya shingo ya kizazi na matiti na kupatiwa elimu ya namna ya kujilinda dhidi ya magonjwa hayo.
Uchunguzi huo umefanyika jana wakati wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group walipokuwa wakiadhimisha siku ya wanawake duniani katika viwanja vya Hospitali hiyo iliyopo TAZARA jijinin Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa hafla ya maadhimisho hayo mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka kutoka Bakhresa Group of Company Mwanafumo Mohamed alisema ni muhimu jamii ikatumia fursa kama hizo zinapojitokeza ili iweze kujifahamu na kuchukua hatua mapema kabla ya kukutwa na changamoto za kiafya.
“Tunatakiwa kuwa na utamaduni wa kutembelea vituo vya afya na kupima afya zetu mara kwa mara kwani kwa kufanya hivyo kutatusaidia kuyagundua mapema magonjwa haya na kutafuta matibabu mapema”, alisema Mwanafumo
Aidha Mwanafumo aliwapongeza wanawake wa Hospitali hiyo kwa kuwa mstari wa mbele kuchochea maendeleo ya Hospitali kwa kufanya shughuli za kijamii zinazoitambulisha Hospitali kwa wadau mbalimbali.
“Huduma mnazozitoa hapa zimejitosheleza, Tunahitaji kuungana kwa pamoja kuhakikisha tunaikuza Hospitali hii hivyo nawaomba wadau mbalimbali nchini mjitokeze tushirikiane kuongeza upanuzi wa Hospitali hii pamoja na kuwekeza vifaa tiba kwani Hospitali hii inawasaidia wagonjwa wa Temeke, Ilala na wengine kutoka wilaya zote za Dar es Salaam”, alisema Mwanafumo.
Kwa upande wake Meneja Rasilimali Watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Abdulrahman Muya aliwapongeza wanawake wa Hospitali hiyo kwa kujitolea kutoa huduma kwa wanawake wenzao, kutoa elimu itakayoisaidia jamii kubadilika na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa wanaotibiwa na Hospitali hiyo.
Muya alisema wanawake wa Hospitali ya JKCI Dar Group wamewaonesha umuhimu wa kuungana kwa pamoja na kufikia malengo kwani kupitia muunganiko wao waliouanzisha rasmi mwezi septemba mwaka jana wameweza kuadhimisha siku hiyo kwa mafanikio makubwa.
“Huu ni mwanzo mzuri, ni matumaini yangu mtaendelea kuwasogezea huduma wananchi ili waweza kupata fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa haya makubwa yanayoisumbua jamii yetu bila ya kuchoka”, alisema Muya
Naye mwenyekiti wa umoja wa wanawake Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Agnes Mkama alisema mwitikio wa jamii kujitokeza kupima magonjwa ya saratani unaonyesha kuwa wanawake wengi wanatambua umuhimu wa kufatilia afya zao.
Agnes alisema magonjwa ya saratani yamekuwa yakiwakumba wanawake wengi nchini na wengi wao hupata dalili wakiwa katika hatua mbaya jambo ambalo limewafanya wanawake wengi kufika katika Taasisi hiyo kufanyiwa uchunguzi.
“Wanawake wanatakiwa kujitokeza kufanya uchunguzi wa afya hasa katika magonjwa yasiyoambukiza kwani kwa kufanya hivyo watakuwa katika wakati mzuri wa kupata matibabu mapema ama kwa wale ambao hawajapatwa na magonjwa haya watakuwa katika nafasi nzuri ya kujilinda”, alisema Agnes
“Nawahasa wanawake wenzangu kufanya uchunguzi wa saratani angalau kila baada ya miaka mitatu, kwani magonjwa ya saratani yakigundulika mapema kuna uwezekano mkubwa wa kupona kabisa tofauti na yanapogundulika katika hatua za kuchelewa”, alisema Agness
Katika maadhimisho hayo wanawake waliojitokeza wameweza kupatiwa huduma mbalimbali ikiwemo kufanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa shinikizo la damu, sukari kwenye damu, saratani ya matiti, saratani ya mlango wa kizazi pamoja na ushauri nasaha na msaada wa kiafya.





