_Akemea ucheleweshaji wa miradi, asema fedha za maendeleo si siri_
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Rukwa kufuatia taarifa za kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi hiyo.
Ametoa agizo hilo leo Jumapili (Machi 8, 2026) wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa Laela mkoani Rukwa baada ya kupokea taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika eneo hilo.
Dkt. Mwigulu amesema Serikali haitavumilia kuona miradi ya maendeleo ikicheleweshwa wakati fedha zake tayari zimetolewa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
“Kamanda wa TAKUKURU nifanyie uchunguzi wa kina, senti mpaka senti, yeyote aliyehusika kwenye hii fedha hapa nipe taarifa hiyo ili niweze kufanya maamuzi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameonesha kutoridhishwa na kuchelewa kwa utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule za sekondari, madarasa pamoja na miundombinu mingine ya elimu katika eneo hilo.
Amesema miradi hiyo imepokea fedha kutoka Serikali lakini utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua, jambo ambalo halikubaliki kwani wananchi wanahitaji kuona matokeo ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo yao.
Aidha, Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa fedha za miradi ya maendeleo hazipaswi kufanywa siri na kwamba taarifa za fedha hizo zinapaswa kuwafikia viongozi mbalimbali wa Serikali ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Msifanye fedha za miradi ya maendeleo kuwa siri. Fedha zikishafika nakala iende kwa Mkuu wa Mkoa, na zikishatumwa kwenye halmashauri nakala apewe Mkuu wa Wilaya na Mbunge, ili kuwe na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa miradi hiyo,” amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watendaji watakaobainika kuchepusha au kutumia vibaya fedha za miradi ya maendeleo kwa kuwa fedha hizo ni mali ya umma na zinapaswa kutumika kwa manufaa ya wananchi.





