WANANCHI wa kata ya Sitalike katika Halmashauri ya Nsimbo wilaya ya Mpanda mkoani Katavi wamewasilisha malalamiko yao kwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba kuhusu baadhi ya watendaji katika wilaya hiyo kutofanyakazi zao kwa weledi hivyo kukwamisha maendeleo.
Wamesema hali hiyo imekuwa ikisababisha kuchelewa au kukosekana kwa haki katika kushughulikia masuala yanayowahusu na kuwalazimu kufuatilia kwa muda mrefu baadhi ya huduma muhimu. “Mara kadhaa tumekuwa tukifikisha malalamiko yetu kwa watendaji husika, lakini baadhi ya masuala yamekuwa yakichelewa kushughulikiwa”.
Malalamiko hayo yaliwasilishwa kwa Waziri Mkuu leo Jumamosi, Machi 14, 2026 na Fainel Maganga ambaye ni mmoja wa wananchi hao alipokuwa akizungumza na wananchi baada ya kukagua Daraja la Mto Katuma katika kaya ya Sitalike, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Katavi.
Maganga amesema hali hiyo imekuwa ikisababisha kupungua kwa imani ya wananchi kwa baadhi ya watumishi wa umma, huku akisisitiza umuhimu wa watendaji hao kuwajibika ipasavyo ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati na kwa usawa.
Aidha, mwananchi mwingine Christopher Luhamba wametumia fursa hiyo kuiomba Serikali kushughulikia changamoto ya kimazingira inayotokana na wachimbaji kumwaga kemikali kwenye mto hali inayohatarisha usalama wao pamoja na viumbe wa kwenye mto Katuma.
Pia wananchi hao wamelalamikia kutopata maeneo ya uchimbaji katika maeneo yao, wakisema hali hiyo imekuwa ikiwanyima fursa ya kujipatia kipato kupitia shughuli za uchimbaji mdogo.
Waziri Mkuu amewataka watendaji kutekeleza majukumu yao na kuwahudumia wananchi kwa sababu moja ya malengo ya Serikali kuwapeleka kwenye maeneo hayo ni kuwahudumia wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Vilevile Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Madini, Anthony Mavunde kufika katika kata yaa Sitalike kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge kwa ajili ya kushughulikia kero ya uchimbaji. Waziri Mkuu ametoa agizo hilo kutokana na kuwepo kwa malalamiko mengi ya masuala ya uchimbaji madini.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekagua Daraja la Sitalike katika mto Katuma, lililopo katika Halmashuri ya Nsimbo mkoani Katavi, ambalo linaunganisha mkoa huo na maeneo mengine ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na nchi jirani ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Rwanda.
Akizungumza baada ya kukagua daraja hilo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo unakwenda kubadilisha historia ya usafiri katika maeneo haya. “Daraja hili limeweka tofauti na lile lililokuwepo awali ambalo halikuwa imara na lilikuwa likisababisha changamoto kwa wananchi na wasafirishaji”.
Ameongeza kuwa Daraja la Sitalike ni sehemu ya miradi ya madaraja inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuokoa maisha ya wananchi, kurahisisha usafiri na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Ujenzi wa Daraja hilo ambalo limeshakamilika kwa asilimia 100 limegharimu shilingi bilioni 9.1 na limejengwa na Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).


