WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, leo Machi 14, 2026 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Jengo la Taaluma na Bweni la wanafunzi katika Kampasi ya Mizengo Pinda ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi.

Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 17.4 unahusisha ujenzi wa jengo la taaluma lenye kumbi za mihadhara na maabara mbalimbali, ambalo linatarajiwa kuhudumia wanafunzi takribani 2,000 kwa wakati mmoja, pamoja na bweni litakalokuwa na uwezo wa kulaza wanafunzi 400.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Nchemba amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha taasisi za elimu ya juu nchini ili kutoa fursa zaidi za elimu kwa vijana wa Kitanzania.
Aidha, aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili kufanikisha ndoto zao na kuwa zawadi kwa wazazi wao na Taifa kwa ujumla. Pia alitoa wito wa kuendelea kumuombea Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, ambaye kampasi hiyo imepewa jina lake kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya elimu nchini.


