RAIS Samia Suluhu Hassan amewapongeza umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi CCM (UVCCM) kwa kufanya matembezi ya pamoja ya vijana zaidi ya 2000 waliotoka Butiama na kutembea hadi jijini Mwanza katika kuenzi kuadhimishamiaka 25 ya kumbukizi ya Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere.
Safari hiyo ya vijana zaidi ya 2000 ilianza Oktoba 09, 2024 kijiji cha Mwitongo wilayani Butiama mkoa wa Mara na hatimaye kuhitimisha katika Uwanja wa CCM Kirumba uliopo wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza Oktoba 14, 2024.
Ameyasema hayo juzi wakati wa kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024,Rais Samia aliwapongeza vijana hao kwa walichokifanya wakiishi falsafa ya Mwalimu Nyerere huku pia akiwapongeza UVCCM kwa kuwalea na kuwaongoza vyema vijana nchini.
Vijana hao walitembea zaidi ya kilometa 200 kuenzi miaka 25 ya Baba wa Taifa, Hayati Nyerere walianza safari yao ambapo matembezi hayo walipita maeneo mbalimbali ikiwemo wilaya za mkoa wa Simiyu, Mara na Mwanza.
Mbali na matembezi hayo waliweza kuhamasisha ushiriki wa vijana katika kujiandikisha kwenye daftari la Mkaazi ili kuweza kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kupanda miti, kuadhimisha wiki ya vijana na kutoa elimu ya uzalendo.