Na Nihifadhi Abdulla
Katika kijiji cha Uzi, kilichopo wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, wanawake wameanza kuandika historia mpya kupitia kilimo mseto. Kijiji hiki, ambacho kipo umbali wa kilomita 34 kutoka Mji Mkongwe wa Zanzibar, kinafahamika kwa utulivu wake, mandhari ya asili, na njia yake ya kipekee ya kufikika wakati wa maji kupwa.
Kwa muda mrefu, uchumi wa Uzi umekuwa ukitegemea uvuvi kwa wanaume, huku wanawake wakijihusisha na kilimo cha kimazoea. Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya tabianchi, hali ya hewa isiyotabirika imeleta changamoto kubwa kwa wakulima, hasa wanawake. Hii imesababisha haja ya mbinu mpya na endelevu za kilimo mojawapo ikiwa ni kilimo mseto.
Kilimo Mseto na Faida Zake
Kilimo mseto ni mfumo wa kilimo ambapo mazao tofauti yanapandwa kwa wakati mmoja au kwa mpangilio maalum, jambo linalosaidia kuongeza mavuno, kuboresha rutuba ya udongo, na kupunguza magonjwa na wadudu waharibifu. Zaidi ya hayo, mbinu hii inasaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kufanya mashamba yao kuwa na kinga dhidi ya hali mbaya ya hewa kama ukame na mafuriko.
Shaaban Peter, Afisa wa teknolojia na uzalishaji katika mradi wa Zanzibar Women in Climate Adaptation (ZAN-ADAPT), anabainisha kuwa kilimo mseto kimekuwa suluhisho muhimu kwa wanawake wa Uzi.
“Kilimo mseto siyo tu kwamba kinaongeza tija kwa wakulima, bali pia kinasaidia kuhifadhi mazingira kwa kupunguza matumizi ya kemikali hatari. Wanawake wa Uzi sasa wanajifunza mbinu hizi na kuzitumia katika mashamba yao,” anasema Peter.
Wanawake na Mapambano Dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi
Tafiti nyingi zimebaini kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaathiri wanawake kwa kiasi kikubwa zaidi kuliko wanaume. Shirika la Oxfam, katika ripoti yake ya mwaka 2017 “An Economy That Works for Women,” lilieleza jinsi wanawake wanavyoathirika kiuchumi na mabadiliko haya, huku likisisitiza umuhimu wa kuwajumuisha katika mipango ya kukabiliana na hali hii.
Vilevile, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women) kwa kushirikiana na UNDP, lilitoa ripoti mwaka 2020 “Jinsia, Tabianchi, na Usalama,” ambayo inaeleza mchango wa wanawake katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuleta amani katika maeneo yaliyo hatarini zaidi.
Amina Rashid ni miongoni mwa mwanawake wa Uzi alioamua kuchukua hatua na kueleza alivyoanza safari yao ya kutumia kilimo mseto kama njia ya kujikimu na kulinda mazingira.
“Awali, tulikuwa tukilima kwa mazoea bila kujua athari zake kwa udongo na mazingira. Lakini baada ya kupata mafunzo kuhusu kilimo mseto, sasa tunaweza kutumia ardhi yetu kwa ufanisi zaidi na kupata mavuno bora,” anasema Amina Rashid.
Mikakati ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi
Wanawake wa Uzi wameanza kutumia maarifa ya kienyeji pamoja na mbinu za kisasa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Shaaban Peter anafafanua jitihada zilizochukuliwa tangu kuanza kwa mradi wa ZAN-ADAPT, ikiwa ni pamoja na mafunzo, usambazaji wa mbegu bora, na uanzishaji wa vikundi vya wakulima.
“Tunalenga kuhakikisha kuwa wanawake wanapata rasilimali wanazohitaji ili kuendesha kilimo chenye tija. Pia tunawahamasisha kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kilimo chao kinakuwa endelevu,” anasema Peter.
Anaongezea kuwa mikakati mingine inayotekelezwa ni pamoja kuimarisha usawa wa kijinsia katika mipango ya kilimo na mazingira kwa kutoa msaada wa kifedha na mitaji kwa wakulima wa wanawake.
Sheha wa kijiji cha Uzi, Malik Mbarak Makame, anaeleza umuhimu wa kushirikiana na wanawake katika kuhakikisha maendeleo endelevu ya jamii.
“Jamii yetu inawategemea wanawake kwa kiasi kikubwa. Tunahitaji kuwaunga mkono ili waweze kuleta mabadiliko ya kweli katika sekta ya kilimo na utunzaji wa mazingira,” anasema Makame.
Matumaini ya Wanawake wa Uzi
Eshe Abdalla anasema licha ya changamoto wanazokumbana nazo, wanawake wa Uzi wana matumaini makubwa juu ya mustakabali wao “kupitia kilimo mseto. tunaimani kuwa mfumo huu wa kilimo utatusaidia siyo tu kuongeza kipato, bali pia kulinda mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi”
Anaendelea kuwa kilimo mseto kitakuwa ngazi ya ustawi kwa wanawake wa Uzi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. “ikiwa juhudi hizi zitaungwa mkono zaidi, bila shaka tutakuwa vinara wa mabadiliko endelevu, siyo tu Zanzibar bali Afrika kwa ujumla”anasema Eshe
Benki ya Dunia, katika ripoti yake ya mwaka 2018 “Gender Equality and Development in a Warming Climate,” ilieleza kuwa ushiriki wa wanawake katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unaweza kusaidia kuongeza uwezo wa jamii nzima kukabiliana na changamoto hizi.
Mradi wa ZAN ADAPT unafadhiliwa na Global Affairs kutoka Canada na kutekelezwa na Community Forests International (CFI), Community Forests Pemba (CFP), kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA-ZNZ