FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu Maalum wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), utakaofanyika katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, kuanzia tarehe 3 hadi 5 Aprili 2025.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Morogoro leo Februari 7, 2025, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema mkutano huo utawakutanisha wanachama wote wa TEF kwa ajili ya kufanya uchaguzi wa viongozi wa jukwaa hilo.
Balile ameongeza kuwa TEF itahakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki, ikiwa ni sehemu muhimu ya taasisi na vyama kujifunza namna bora ya kuendesha chaguzi za kidemokrasia.
Amefafanua kuwa uchaguzi huo unafanyika kwa mujibu wa Ibara ya 7 na Ibara ndogo ya 8 ya Katiba ya TEF, ambapo muda wa uongozi wa sasa unafikia tamati baada ya kutumikia kwa miaka minne tangu mwaka 2021.
Katika uchaguzi huo, wanachama watawachagua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, pamoja na wajumbe saba wa Kamati Tendaji ya TEF.
Aidha amesema fomu za kuomba nafasi za uongozi zitaanza kutolewa rasmi Jumatatu, Machi 10, 2025, katika ofisi za TEF zilizopo Mtaa wa Mtendeni, Kisutu, jijini Dar es Salaam huku mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni Machi 24, 2025, ifikapo saa 10:00 jioni.
Wagombea wanatakiwa kurejesha fomu zao wakiwa na picha moja ndogo (passport size), ambayo itatumika kwenye karatasi za kura endapo watachaguliwa kuwania nafasi wanazoomba.
Pia muda wa kuchukua na kurejesha fomu ni kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni katika siku za kazi pekee. “Fomu hazitatolewa wala kupokelewa siku za Jumamosi, Jumapili, na sikukuu”. Amesema Balile
Amesema Kwa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ada ya fomu ni shilingi 150,000, huku ada kwa nafasi za wajumbe wa Kamati Tendaji ikiwa ni shilingi 100,000 huku akisisitiza Kuwa ada hizi hazitarejeshwa endapo mgombea atabadili mawazo.
Uchaguzi huo utasimamiwa na Kamati ya Uchaguzi inayoongozwa na Frank Sanga kama Mwenyekiti, pamoja na wajumbe Angel Mang’enya na Rashid Kejo. Kamati hii ina jukumu la kuhakikisha taratibu zote za uchaguzi zinafuatwa, ikiwa ni pamoja na vigezo na sifa za wagombea.
Kaulimbiu ya mkutano huo ni ‘Uchaguzi Huru na wa Haki.’.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi