Na Said Mwishehe,Michuzi TV
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kimegoma kusaini Kanuni za maadili ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani za mwaka 2025 na hivyo Chama hicho kitakuwa kimekosa sifa ya kushiriki uchaguzi huo.
Akizungumza na Waandishi wa habari ,Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Ramadhani Kailima amefafanua kuwa chama ambacho hakijasaini kanuni za maadili hayo hakitopata fursa ya kushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka huu wa 2025 pamoja na chaguzi ndogo zote ambazo zitatokea ndani ya miaka mitano.
Kailima amesema kuwa vyama vyote vya siasa vilipewa taarifa kuhusu kufika Aprili 12 mwaka huu kusaini kanuni za maadili ambazo huqndaliwa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi mkuu na vyama 18 vimefika lakini Chama kimoja hakijafika licha ya kuwa tayari walishapewa taarifa.
“Tulitoa taarifa ya kuzungumza na vyama vyote vya siasa ambavyo vitashiriki uchaguzi Mkuu ,vyama 18 vimekuja lakini chama kimoja licha ya kuzungumza na viongozi wake lakini hawajafika.
“… lakini ifahamike chama ambacho hakijasaini leo hakitashiriki uchaguzi Mkuu.Na kusaini ilikuwa leo hivyo hatutarajii Chama ambacho hakijasaini kuja siku nyingine maana kusaini ilikuwa ni leo Aprili 12,2025.”
Kailima akifafanua mambo muhimu yaliyomo kwenye kanuni hizo amesema vyama vya siasa vina wajibu wa kufanya kampeni za kistaarabu na kujiepusha na mambo yanayoweza kupelekea uvunjifu wa amani.
Ameongeza Serikali kwa upande wake ina wajibu wa kutoa fursa sawa ya vyama vya siasa kufanya kampeni, kutumia vyombo vya habari vya umma na kuhakikisha kuwa kunakuwepo na hali ya utulivu na amani.
“Kwa upande wa Tume inawajibika kwenye mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa huru na wa haki na kuhakikisha kunakuwa na usawa katika mchakato wa uchaguzi.”
Vyama ambavyo vimesaini kanuni hizo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Civic United Front (CUF), National Convention for Construction and Reform (NCCR), Union for Multiparty Democracy (UMD), National League for Democracy (NLD), United Peoples’ Democratic Party (UPDP) na National Reconstruction Alliance (NRA), African Democratic Alliance Party (ADA-TADEA).
Vyama vingine ni Tanzania Labour Party (TLP), United Democratic Party (UDP), Madini Kilimo Nishati (MAKINI), Democratic Party (DP), Sauti ya Umma (SAU), Alliance for African Farmers Party (AAFP), Chama cha Kijamii (CCK), Alliance for Democratic Change (ADC) na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) na Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo).
Kwa upande wa Serikali Kanuni hizo za maadili zilisainiwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi na kwa upande wa Tume alisaini Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani, Mhe. Jacobs Mwambegele.
Awali akizungumza kabla ya utiaji saini, Jaji Mwambegele alivishukuru vyama vya siasa kwa ushirikiano wao wakati wote wa uandaaji wa kanuni hizo za maadili.
“Tunawashukuru viongozi wote wa Vyama vya Siasa kwa namna ambavyo mmekuwa mkiipa ushirikiano Tume katika utekelezaji wa majukumu yake mbalimbali hususan yale yanayohusu mchakato wa maandalizi ya uchaguzi…
“Ikiwemo uandaaji wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi ambazo tupo hapa leo kwa ajili ya kutia saini kwa ajili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2025,” amesema Jaji Mwambegele.
Ameongeza Tume imeandaa kanuni hizo za maadili ambazo zitatambulika kama Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025 kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Na. 1 ya Mwaka 2024.
“Baada ya kukamilisha maandalizi ya rasimu ya Kanuni hizo, Tume iliziwasilisha kwenu (vyama vya siasa na Serikali) kwa ajili ya kupitia na kutoa maoni yenu kuanzia tarehe 1 Machi, 2025 hadi tarehe 14 Machi, 2025.
Maoni yenu yamejumuishwa katika Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 tutakazotia saini hii leo. Napenda kutoa shukrani za dhati kwenu kwa ushiriki wenu katika kuandaa rasimu hiyo kwa kutoa maoni yenu na kuyawasilisha Tume kwa wakati,” amesisitiza Jaji Mwambegele.
Ameongeza baada ya kukamilisha rasimu ya Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025, Tume iliwarejeshea tena wahusika Rasimu ya Kanuni hizo tarehe 4 Aprili, 2025 na kuwaalika kwa ajili ya utiaji saini leo tarehe 12 Aprili, 2025 na kwamba hakuna maoni tofauti yaliyotolewa.