Na Pamela Mollel, Arumeru
Joto la uchaguzi katika Jimbo la Arumeru Magharibi, mkoani Arusha, limeendelea kupanda huku wagombea wakijitokeza kuchukua na kurejesha fomu za kuwania uteuzi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Miongoni mwa waliorejesha fomu ni Elias Lukumay, kada maarufu wa chama hicho na Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), aliyefanya hivyo Julai 2, 2025.
Aidha, kada kindakindaki wa CCM, John Tanaki, naye amejiunga katika kinyang’anyiro hicho, akijizolea umaarufu kupitia mitandao ya kijamii kwa kauli yake ya kutaka “kuiweka dunia kuwa mahali salama pa kuishi.”
“Nimeanza safari hii kupitia familia yangu. Tukitaka kubadilisha dunia, ni lazima tuanze kwa mtu mmoja mmoja hadi familia,” alisema Tanaki.
Alisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kutambua nafasi yao kama wasaidizi wa Rais katika kuleta maendeleo kwa wananchi.