
Mahakama ya Kikatiba ya Thailand imemuondoa madarakani Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Paetongtarn Shinawatra, kufuatia sakata la simu iliyovuja kati yake na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Cambodia, Hun Sen.
Katika mawasiliano hayo ya simu, Paetongtarn alimwita Hun Sen “mjomba” na kisha kutoa kauli za kejeli dhidi ya kamanda wa jeshi la Thailand. Tukio hilo lilizua mjadala mkubwa, ambapo wakosoaji walimshutumu kwa kudhoofisha heshima na nguvu za jeshi, moja ya taasisi zenye ushawishi mkubwa nchini humo.
Baada ya kisa hicho, Paetongtarn aliomba radhi akieleza kuwa maneno yake yalikuwa sehemu ya “mbinu ya mazungumzo” kutokana na mvutano unaoendelea katika mpaka wa Thailand na Cambodia.
Hata hivyo, mahakama ilibaini kuwa vitendo vyake vilikinzana na maadili ya kitaifa na kuzingatia zaidi maslahi binafsi, hivyo kuvunja viwango vya uadilifu vinavyohitajika kwa kiongozi wa taifa.
Katika taarifa yake ya kwanza baada ya hukumu hiyo, Paetongtarn alikiri matokeo ya uamuzi huo lakini akasema yamezua “mabadiliko mengine ya ghafla” nchini humo, akibainisha kuwa sasa anakuwa Waziri Mkuu wa tano kuondolewa madarakani na mahakama tangu mwaka 2008.