Baadhi ya wanafunzi wanufaika wakiwemo wazazi, leo wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupokea msaada wa vifaa vya shule.Nyuma wa pili kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Alhaji Dk.Sibtain Meghjee na Sheikh wa Shia Ithna Asheri, Kanda ya Ziwa, Sheikh Hashimu Ramadhan .Bernadeta Ngeleja mwenye ulemavu wa miguu na mkono (aliyekaa kwenye kiti mwendo), kwa niaba ya wajukuu wake, leo, akipokea msaada wa vifaa vya shule kutoka kwa Mwenyekiti The Desk & Char Foundation, Alhaji Dk.Sibtain Meghjee (kushoto) , anayeshuhudia ni Sheikh Hashim Ramadhan, wa Shia Ithna-Sheri. Picha zote na Baltazar Mashaka

Bernadeta Ngeleja mwenye ulemavu wa miguu na mkono (aliyekaa kwenye kiti mwendo), kwa niaba ya wajukuu wake, leo, akipokea msaada wa vifaa vya shule kutoka kwa Mwenyekiti The Desk & Char Foundation, Alhaji Dk.Sibtain Meghjee (kushoto) , anayeshuhudia ni Sheikh Hashim Ramadhan, wa Shia Ithna-Sheri. Picha zote na Baltazar Mashaka
Mwanafunzi wa Kakebe sekondari ambye ni yatima, Hamis Kibugwa (kushoto), akipokea msaada wa madaftari kutoka kwa Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Alhaji Dk.Sibtain Meghjee, leo jijini Mwanza.
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
*Wazazi Mwanza waomba serikali kugharamia vifaa vya elimu kwa wanafunzi
TAASISI ya The Desk & Chair Foundation, leo imeendelea kutoa msaada wa vifaa vya elimu kwa zaidi ya wanafunzi 500 wa shule za msingi na sekondari jijini Mwanza, ili kuwaondolea changamoto wenye uhitaji waendelee na masomo bila vikwazo.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Alhaji Dk. Sibtain Meghjee, alisema msaada huo ni endelevu na unalenga kuhakikisha wanafunzi wote wanaokosa vifaa muhimu vya shule hawapotezi fursa ya kupata elimu ambapo kwa miaka 10, taasisi hiyo imekuwa ikisaidia jamii na familia duni zisizo na uwezo wa kugharamia mahitaji ya shule kwa watoto wao.
“Taasisi yetu kwa zaidi ya miaka 10 imekuwa ikitoa msaada kwa jamii, hususan familia duni zisizo na uwezo wa kununua mahitaji ya shule kwa watoto wao. Wahitaji ni wengi, lakini tutaendelea kuwafadhili licha ya changamoto ya upatikanaji wa wafadhili,” alisema Dk. Meghjee.
Alieleza kuwa awamu hii ya pili ya msaada imewahusisha wanafunzi zaidi ya 500 wa shule za msingi na sekondari jijini Mwanza, huku katika awamu ya kwanza wanafunzi 1,000 wakinufaika kwa kupatiwa vifaa vya elimu bila malipo.
Kwa upande wake, Hamisi Kibugwa, yatima na mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Kakebe, alisema baada ya kufiwa na wazazi wake anaishi maisha ya dhiki pamoja na babu na bibi yake, hali inayowafanya washindwe kumudu mahitaji ya shule.
“Ili kupata fedha za kujikimu, babu na bibi walikuwa wakiuza udongo (pemba), lakini sasa hawana mtaji. Naiomba serikali iigharamie vifaa vya shule kwa wanafunzi wasio na uwezo baada ya kutambuliwa, ili tuondokane na changamoto ya kukosa vifaa vya elimu,” alisema na kuishukuru The Desk & Chair Foundation kwa msaada huo, ingawa mahitaji yake bado, ana uhitaji wa madaftari mengine saba.
Aidha, baadhi ya wazazi wameiomba serikali ya awamu ya sita kuangalia uwezekano wa kutenga fedha au kutafuta vyanzo maalum vya kugharamia vifaa vya elimu, ili watoto waweze kupata elimu bila vikwazo.
Walisema kuwa katika miaka ya 1970, elimu ilitolewa bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu, ambapo wazazi waligharamia sare pekee, huku wanafunzi wakisafiri kwa hati maalum kwenda shule za sekondari na vyuo, kikiwemo chuo kikuu.
Hata hivyo, walieleza kuwa mabadiliko ya kiuchumi na utekelezaji wa sera za Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) za miaka 1980, hususani kuanzia 1985 (Mpango wa Marekebisho ya Uchumi), ziliifanya serikali ijiondoe kugharamia elimu na huduma zingine za jamii kama afya bure .
“Elimu ilikuwa bure kabisa isipokuwa sare za shule. Mpango wa usafiri kwa wanafunzi ulikuwepo, lakini ulifutwa baada ya mageuzi ya kiuchumi. Sera hizo zililenga kusaidia nchi zilizokuwa na matatizo makubwa ya kiuchumi, ikiwemo Tanzania, kwa kutoa mikopo na misaada ya kifedha kwa masharti maalum,” alisema mmoja wa wazazi kwa hifadhi ya jina.
Alieleza kuwa, miongoni mwa masharti hayo ilikuwa kupunguza matumizi ya serikali katika huduma za jamii kama elimu na afya, kujiondoa kwa serikali kugharamia huduma zote kikamilifu,kuhamasisha mchango wa wananchi katika huduma za kijamii.
“Kutokana na masharti hayo, serikali ya Tanzania iliacha sera ya elimu bure, ambayo hapo awali iligharamia ada za shule,ununuzi wa vifaa vya elimu ( vitabu, madaftari na vifaa vya kufundishia),kulipia gharama nyingine za uendeshaji wa shule,” alisema mzazi huyo.
Aliongeza kuwa, badala yake, wazazi na walezi walianza kuchangia gharama za elimu, ikiwemo kununua vifaa vya shule na kulipa ada mbalimbali, hatua hiyo ililenga kupunguza mzigo wa kifedha kwa serikali lakini ilisababisha kupungua kwa uandikishaji wa wanafunzi, hasa kutoka familia maskini.
Kuongezeka kwa tofauti za kielimu kati ya matajiri na maskini na kushuka kwa ubora wa elimu katika baadhi ya maeneo, hivyo sera za Benki ya Dunia na IMF za mwaka 1985 zilichangia kuondolewa kwa elimu bure nchini, zikiakisi mabadiliko ya sera za kiuchumi kutoka mfumo wa ujamaa kwenda uchumi wa soko huria.
Walisema pamoja na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kufanya maboresho makubwa katika sekta ya elimu, hususan katika ujenzi wa miundombinu, ipo haja ya serikali kuangalia suala la vifaa vya elimu.
“Rai yangu serikali iangalie namna ya kugharamia vifaa vya elimu ili kuwaondolea watoto changamoto hiyo, wasome kwa kupata maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya jamii.Pia, niwashukuru The Desk & Chair Foundation kutoa vifaa vya elimu bure,masharika na taasisi ziige kusaidia jamii ,” alisema Alex Nyawambo, mkazi wa Kanyerere.
“Niipongeze taasisi ya The Desk & Chair Foundation, kwa kufadhili watoto wenye uhitaji waliopo shuleni, ni msaada mkubwa kwa watoto wa Kitanzania kuhakikisha wanapata elimu bila kikwazo,”lisema Tawfiq Ali, mkazi wa Isamilo .
Waliongeza kuwa serikali inaweza kutenga fedha za ruzuku ya vifaa vya elimu kama ilivyofanya kwa waagizaji wa mafuta, hatua itakayopunguza mzigo wa gharama za elimu kwa wazazi ambao ni walipa kodi wakubwa.



.jpeg)


