WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),imezifutia usajili Kampuni 11 ambazo zimekiuka masharti ya Kifungu cha 400A (1) (e) cha Sheria ya Kampuni Sura 212 kwa kufanya shughuli za kibiashara nje ya madhumuni yaliyoainishwa katika Katiba za kampuni hizo na miongozo ya uendeshaji wa kampuni wakati wa usajili.
Kampuni hizo ni pamoja na LBL Mtwara Media Company Limited (Na. 181289972), LBL Morogoro Media Company Limite1d (Na. 179770873), LBL Geita Advertising Media Limited (Na. 180439242), LBL Mbeya Media Limited (Na. 179978326),LBL Future Vision Advertising Agency Company Limited (Na. 181302259),
Nyingine ikiwa ni LBL Mbezi Advertising Media Company Limited (Na. 180582835),LBL Ubungo Media Limited (Na. 180960333),LBL Mabibo Media Company Limited (Na. 181117346),LBL Mbagala Media Company Limited (Na. 181248874) ,LBL Gongo la Mboto Media Advertising Company Limited (Na. 181513438) na LBL Dar es Salaam Kigamboni Advertising Company Limited (Na. 180046992).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 5, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa BRELA Godfrey Nyaisa, amesema kwamba kampuni hizo zimekiuka masharti kwa kufanya shughuli za kibiashara tofauti na madhumini yaliyoainishwa katika katiba za kampuni za miongozo ya uendeshaji wake wakati wa usajili
Amefafanua kuwa kutokana na kampuni hizo kutowasilisha maelezo yoyote kama zilivyotakiwa chini ya kifungu cha 400A (2), Msajili amezifuta rasmi na hatua nyingine za kisheria zimeanza kuchukuliwa na vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa wahusika ikiwemo kuwatia nguvuni.
“Napenda kuwasisitiza kwamba hakuna kampuni na wahusika wake watakaokuwa salama ikiwa watakiuka sheria na taratibu wa usajili wa kampuni, kampuni yoyote ile itakayofanya shughuli zake kinyume na sheria na utaratibu itashughulikiwa ipasavyo na vyombo vya usalama.
Nyaisa amesema kuwa hakuna sheria wala taasisi yenye mamlaka ya kutoa vibali wala leseni za kufanya biashara za upatu hapa nchini.
Nyaisa amesema biashara ya upatu ni kinyume na sheria za nchi na hivyo wananchi wanahimizwa kutoa taarifa mara moja kwa Mamlaka husika, zikiwemo taasisi za Kiserikali na Jeshi la Polisi, ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya kampuni au watu wanaofanya au kujihusisha na biashara hiyo.